HUU HAPA MFUMO BORA WA KUMILIKI MALI KWA WANANDOA

 


Picha na  Mtandaoni

Tatizo kubwa katika ndoa nyingi limekuwa sio namna ya kuzipata mali bali namna ya kuzimiliki. Japokuwa mchakato wa umiliki unaweza ukaathiriwa na mchakato wa upatikanaji wa mali zenyewe, lakini mara nyingi matatizo na migogoro mingi imejitokeza baada mali hizo kupatikana. 


Watu wengi wamekuwa wakijiuliza, je ni mfumo upi unaofaa kiuchumi na kisheria katika umilikaji wa mali tulizonazo kama wanandoa? Je mali ambazo zimepatikana kwa mchango wa moja kwa moja wa mume, mke ana haki ya kuzimiliki? Je mali ambazo mke amezipata kibinafsi kwa jitihada zake binafsi mume ana haki ya kuzimiliki? 


Mume ana haki kumiliki nyumba iliyojengwa na mkewe? Je mume ana nafasi gani katika biashara iliyoanzishwa na kuendelezwa na mkewe? Kuna maswali mengi tumejiuliza lakini makala hii inaweza kukupa majibu ya maswali yako na kukupa ushauri juu ya mfumo bora wa kumiliki mali kwa wanandoa.


Jambo la msingi na la kuzingatia ni kwamba, japokuwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inatoa mwanya wa mwanandoa kumiliki mali kibinafsi, lakini ili kulinda maslahi ya wanandoa wote wawili, sheria imeeleza wazi kuwa mali zitakazochumwa na wanandoa kuanzia siku waliyoanza kuishi pamoja kama wanandoa zitakuwa mali ya wote wawili bila kujali mchango wa mke au mume katika upatikanaji wa mali hizo. 


Kitendo cha kuishi pamoja kama wanandoa ni mchango tosha unaotambulika kisheria katika upatikanaji na umiliki wa mali hizo. Hii haijalishi mali hizo wakati zinanunuliwa zilinunuliwa kwa jina la nani. Pia haijalishi hati za umiliki wa mali hizo zimeandikwa jina la nani. Ili mradi zimepatikana katika kipindi ambacho wanandoa walikuwa wakiishi pamoja mali hizo ni mali za wanandoa wote wawili. 

Hata hivyo kuna utofauti kidogo katika mali zilizopatikana kabla ya ndoa kufungwa, mali za urithi au zawadi ambayo mke au mume anaweza kupewa kibinafsi. Kuifanya mali hiyo iwe ya wote wawili itategemea ridhaa ya mhusika ambaye ni mmiliki.


Ifahamike wazi pia kwamba, kwa kuwa mali hizi ni za wanandoa wote wawili mmojawapo hawezi kuuza, kuweka rehani kwa kuchukua mkopo, kutoa, kummilikisha mtoto au mtu mwingine yeyote pasipo ridhaa ya mwenzake. Chochote kitakachofanyika pasipo ridhaa ya mwenzi wako kuhusiana na mali hizo kitakuwa ni batili kisheria.


Hata hivyo ili kuondoa migogoro, manyanyaso, ubaguzi, ukatili na dhuluma ambayo inaweza kufanywa kwa mke au mume na wanandugu baada ya mmojawapo kufariki, ni vyema umiliki wa makampuni, biashara, magari, nyumba, viwanja, hisa, akaunti za benki na rasilimali mbalimbali ukawa ni umiliki wa pamoja. Majina ya wote wawili yaonekane katika hati za umiliki wa mali hizo. 

Mnaweza pia kuamua kufungua kampuni ambayo wote mtakuwa wamiliki na wakurugenzi wa kampuni hiyo na kisha mali zenu kuzisajili chini ya umiliki wa kampuni hiyo. Hiyo itasaidia kuondoa usumbufu wa mirathi kwa kuwa yule atakayebaki ndiye atakayekuwa mmiliki halali.  


Inafaa sana mke kumshirikisha mume na mume kumshirikisha mke katika maswala yote ya ununuzi na umiliki wa mali. Ukinunua mali kisirisiri utaipoteza kisirisiri. Ukiuza mali au kuikopea kisirisiri utagundulika na utaumbuka na kuhatarisha mahusiano yako. Biashara zote zilizofanikiwa zimejengwa katika msingi wa ndoa bora na mahusiano mazuri yenye ukweli na uwazi kati ya wanandoa.

0/Post a Comment/Comments