Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Njedengwa jijini Dodoma leo Tarehe 27 Agosti, 2021.
......................................................................
TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuwepo kwa nafasi mbili za Ubunge
katika majimbo ya Konde mkoa wa Kaskazini Pemba na Ushetu mkoani Shinyanga.
Akizungumza
na Vyombo vya habari leo tarehe 27 Agosti 2021, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera amesema uchaguzi huo mdogo wa marudio
umepangwa kufanyika Oktoba 9,2021.
“Ratiba ya
uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa
Kaskazini Pemba na Jimbo la Ushetu Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga ipo
tayari,”alisema Dkt. Mahera.
Alisema
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania yenye Kumb. Na. CEA.137/400/02/111 ya tarehe 16 Agosti
2021, akiitaarifu kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la
Ushetu Mkoani Shinyanga.
Nafasi
hiyo inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Elias John Kwandikwa
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dkt Mahera
amesema taarifa hiyo ya Spika ni kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Aidha, kwa
upande wa Jimbo la Konde, Dk Mahera amesema mnamo tarehe 2 Agosti, 2021 Tume ya
Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa umma kuhusu kuwepo wazi kwa Jimbo la
Konde lilipo katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kutokana
na mbunge mteule wa jimbo hilo, Sheha Mpemba Faki kujiuzulu.
“Tume
ilipokea barua yenye Kumb. Na. CMM/T.40/Vol.I/72 ya tarehe 2 Agosti, 2021
kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitoa taarifa kuwa Mbunge
Mteule wa Jimbo la Konde, ameandika barua, kueleza kwamba hakuwa tayari
kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Konde kutokana na changamoto za
kifamilia,”alisema Dkt. Mahera na kuongeza kuwa kutokana na hatua hiyo, Tume
ililitangaza jimbo hilo kuwa wazi kwa kuwa Mbunge huyo Mteule alikuwa bado
hajatangazwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 81(c) (iii)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Awali
mnamo tarehe 18 Julai, 2021 Tume iliendesha Uchaguzi mdogo katika Jimbo la
Konde kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa
jimbo hilo, Khatibu Saidi Haji kupitia chama cha Alliance for Change and
Transparency (ACT –WAZALENDO)
Maandalizi
kwa ajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa
wagombea inaanza Septemba 13 hadi 19,2021 huku uteuzi wa wagombea watakao wania
nafasi hizo ukifanyika Septemba 19 mwaka huu.
Aidha, Dkt
Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika majimbo hayo ya Ushetu na Konde
utaanza Septemba 20, 2021 na zitafikia ukomo wake Oktoba 8 mwaka huu na
uchaguzi kufanyika 9 Oktoba ,2021.
Dk Mahera
amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote
wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo
na maelekezo yatakayotolewa na Tume katika kipindi cha Uchaguzi mdogo.
Post a Comment