Serikali imesema haitavumilia sababu
zinazokwamisha Wazee kupata huduma ya matibabu kama ilivyo katika miongozo na
maelekezo ya viongozi kuhusu huduma kwa Wazee nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Idara Kuu ya
Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema hayo mjini Bukoba Mkoani
Kagera katika ziara yake Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kagera kukagua ya utoaji wa
huduma kwa wazee, wanawake na watoto.
Amesema kuwa maelezo kuhusu baadhi ya
dawa kutotolewa kwa wazee kutokana na maelekezo ya Bima ya Afya yanahitaji
kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili waweze kupata huduma kama ilivyoelekezwa.
“Nimeambiwa kwamba baadhi ya dawa
hazipatikani kwa wazee kwa maelekezo kadhaa kulingana na viwango na uwezo wa
hospitali tusingependa kusikia baadhi ya wazee wanakosa dawa kwa sababu yoyote”
alisema
Aidha, Mhe. Mwanaidi amemuelekeza
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kuwasilisha taarifa ya
upatikanaji wa dawa Wizarani ili kuhakikisha wazee na makundi mengine ya
kipaumbele yanapata huduma stahiki.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwanaidi
alitembelea wodi ya watoto, wajawazito na wazazi na kupata maelezo ya huduma
zinazotolewa hospitalini hapo.
Aidha, amewapongeza watoa huduma
katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuongeza
kwamba kazi hiyo ni ya wito hivyo waendelee kujitoa na kufanya kazi kwa moyo.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza Kiilima nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba na kuiagiza Wizara kuendelea kutoa huduma kwa wazee hao.
Post a Comment