TMA YATOA TAHADHARI ONGEZEKO LA JOTO NCHINI.


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya kuwepo kwa  ongezeko la joto linatokana na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi kama ilivyotabiriwa awali.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa leo kwa vyombo vya habari na Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri TMA Samwel Mbuya amesema kutokana na mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kuonyesha kuwa na mvua chache na kusuasua na kupelekea kuwa na hali ya ukavu imesababisha viwango vya joto kuendelea kuongezeka katika maeneo mbalimbali nchini.

Mbuya amesema vipindi vya jua la utosi hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).

Aidha Mbuya amesema katika kipindi hiko viwango vya joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwa ambapo mkoa wa Kilimanjaro umeripoti kiwango cha juu cha joto ambacho kimefikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.

‘Vilevile, kiwango cha juu cha joto katika mkoa wa Dar es salaam kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika mkoa wa Ruvuma kimefikia nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3.Hali kama hii imejitokeza pia katika mikoa yote nchini ambapo kiwango cha joto kimekuwa kikubwa kuliko wastani wa muda mrefu’amesema Mbuya

Amesema Vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2021 na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2021 ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka sambamba na mionzi ya jua la utosi kuwa imeondoka katika maeneo ya nchi yetu.

Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kujiepusha na madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo joto kali

0/Post a Comment/Comments