Chifu Godfriend Kileo (kushoto) wa Siha akichangia mada wakati wa kikao cha Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi. Kulia ni Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa Kilimanjaro Chifu Frank Mareale wa himaya ya Marangu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu (katikati) akichangia mada wakati wa kikao cha Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi. Kushoto ni Alaigwanani Gabriel Mollel kutoka wilaya ya Hai na kulia ni Chifu Jabiri Msofe kutoka wilaya ya Mwanga.
Na Eleuteri Mangi, WUSM- Moshi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro
ambalo litafanyika Januari 22, 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika
kilichopo Manispaa ya Moshi.
Taarifa ya Tamasha hilo imetolewa na Umoja wa Machifu wa mkoa huo chini
ya Mkuu wa Chifu nchini ambaye pia ni Mkuu wa Chifu wa Mkoa wa
Kilimanjaro Chifu Frank Mareale wa himaya ya Marangu katika katika
kikao cha Machifu wa mkoa huo kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Moshi.
“Ni heshima mkoa wetu kuwa wa kwanza kutekeleza agizo la Chifu Mkuu Rais
Mhe. Samia Suluhu Hassan ambalo alilitoa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba 2021
katika Tamasha la Utamaduni ambalo aliagiza mikoa yote nchini kuendesha
matamasha ya utamaduni kwa lengo la kuelimisha jamii na kuendeleza utamaduni
wetu” amesema Chifu Mareale.
Akizungumzia Tamasha hilo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni kutoka
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu amesema mkoa wa
Kilimanjaro umeitikia agizo la Rais Mhe. Samia Suluhu ambapo alitoa maelekezo
kwa mikoa yote nchini kufanya matamasha ya kiutamaduni katika maeneo yao.
“Tumeanza safari kubwa ya kuimarisha utamaduni wa mkoa wa Kilimanjaro,
Matamasha haya yatainua na kuibua hazina kubwa ya kiutamaduni miongoni mwa
jamii iliyopo nchi nzima itakayotumika kwa manufaa ya tmtu mmoja mmoja na taifa
kwa ujumla na yataleta” amesema Dkt. Temu.
Ili kulifanya tamasha hilo kuwa la jamii nzima, Dkt. Temu amesema kuwa
vijana wahamasishwe kushiriki hatua itakayowasaidia kujifunza na kuonja
uthamani wa utamaduni kama anavyoothamini Rais Samia Suluhu Hassan ambaye
anaonesha kwa vitendo kwa kushiriki matamasha ya utamaduni nchini kudhihirisha
kuwa utamaduni ni utajiri ambao unaweza kuwasaidia watu wote kuanzia vijana
hadi wazee kama chanzo cha ajira kupitia utalii wa kiutamaduni katika maeneo
mbalimbali nchini.
Dkt. Temu amesema kuwa kwa mujibu wa Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997,
wananchi wanawajibu wa kuendeleza utamaduni na Serikali ikiwa na wajibu wa
kusimamia mila na desturi na kuongeza kuwa tamasha la Kilimanjaro linatarajiwa
kuwa na vionjo ambavyo vitakuwa na mvuto kwa watanzania kwa kuonesha vyakula
vya asili vya kutosha, mavazi ya asili, ngoma za asili pamoja na historia ya
makabila ya Wachaga, wapare, wamasai na wagwemo na kuwa tamasha la mfano ambalo
litatoa hamasa kwa mikoa mingine kuandaa matamasha ya kiutamaduni katika mikoa
yao.
Tamasha la Kilimanjaro ni utekelezaji wa Sera ya Utamaduni ambayo imetoa mwelekeo wa maendeleo ya utamaduni kwa kuainisha jinsi shughuli za utamaduni zitakavyoendeshwa na kusimamiwa pamoja na kuweka wazi majukumu ya Serikali, wananchi kwa makundi au mmoja mmoja na sekta binafsi ili kufanikisha lengo la kuhifadhi na kuuenzi utamaduni wetu
Post a Comment