MOI YAANZA KUFANYA UPASUAJI KUONDOA UVIMBE KWENYE SAKAFU YA UBONGO.


...................................

NA MUSSA KHALID,

Taasisi ya Mifupa Muhimbili -MOI imeanza kambi ya kufanya upasuaji wa  kuondoa uvimbe uliopo kwenye sakafu ya Ubongo kichwani ili kuwasaidia watu wenye changamoto hiyo.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa -MOI Dkt Respicious Boniphas amesema katika kambi hiyo madaktari wa Tanzania wanafundishwa mbinu hiyo kutoka kwa madaktari wa Uganda ambao pia ni zao la taasisi hiyo.

Dkt Respicious ameeleza faida ya mbinu hiyo kuwa ni pamoja na kurahisisha muda kuwa mfupi tofauti na ilivyokuwa awali wagonjwa walikuwa wakikaa muda mrefu wodini.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo Aingaya Kaale amesema kuwa takriban  wagonjwa 600 sawa na wastani 30-50 kwa mwezi ambao wamewafanyia upasuaji hivyo malengo yao ni kuwafanyia wagonjwa nane katika wiki moja.

Ramadhan Msuya ni mmoja ya wagonjwa ambaye anatibiwa katika Taasisi hiyo ameeleza kuwa alianza kusumbuliwa na macho lakini wataalamu wa Afya wamemsaidia kwa kumfanyia upasuaji na hivyo kuwa katika hali nzuri.

Hata hivyo  wito umetolewa kwa watanzania kuhakikisha wanakwenda Hospitalini kufanya vipimo wanapojihisi kuumwa hasa dalili zikionyesha vichwa kuuma au macho kutokuona vizuri ili waweze kupata tiba mapema.

0/Post a Comment/Comments