TIC YAWAFUNDA WANANCHI KUHUSU SHERIA YA MIGOGORO NA WAWEKEZAJI.


Mkurugenzi wa maswala ya kitaasisi kutoka –TIC, Suleiman Mnzava  
...................................

Na Issa Mohamed –Dar es salaam

Issamohamed765@gmail.com

Kituo cha Uwekezaji Nchini –TIC kimekusudia kutoa elimu kwa wananchi hasa katika kutambua sheria za uwekezaji pamoja na faida zake za uwekezaji kwenye maeneo yao lengo ni kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza baina yao (wananchi) na wawekezaji.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Maswala ya Kitaasisi kutoka –TIC, Suleiman Mnzava wakati akizungumza na KISS FM ambapo amesema ni wazi kuwa serikali inathamini mchango wa wawekezaji hivyo kutoa elimu hiyo itasaidia kuboresha ujio wa wawekezaji.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 imeoanisha utaratibu wa ulipaji wa fidia endapo mtu anahitaji kununua ardhi hivyo –TIC imeendelea kushauri wawekezaji juu ya ununuzi wa ardhi kati ya mwekezaji na wananchi.

‘’Mfumo wenyewe wa sheria ya uwekezaji umezuia kabisa migogoro kutokana na wawekezaji kupokelewa na TIC, pia kuna kituo cha huduma za mahala pamoja ambacho kinajumuisha taasisi mbalimbali za serikali kama vile  ardhi, NEMC, TBS, BRELA, Uhamiaji ili kumsaidia mwekezaji kupata taarifa zote katika sehemu moja’’ Amesema Mnzava.

Sambamba na hilo Mnzava amesema –TIC inatarajia kuweka utaratibu na kananuni za kimaadili ili kuwasajili mawakala wanaohusika kuwashauri wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini lengo ni kuondoa vishoka.

‘’Kituo kipo katika hatua za mwisho katika kuanzisha kanuni za kuwasajili watu watakaoshughulika na wawekezaji kwani hapo awali walikua hawajulikani kutokana na wawekezaji kuhitaji watu makini’’ Ameongeza Mnzava.

Aidha amesema kuwa kituo hicho kinatarajia kukutana na chama cha mawakili nchini mwezi huu wa Juni ili kujadili sheria hizo huku zikitarajiwa kutumika kabla mwezi Julai/Agosti mwaka huu.

Ameongeza kuwa TIC imesaini mikataba na makampuni takribani sita yaliyokuja kuwekeza uwekezaji mahiri maalumu kuanzia dola za marekani milioni 150 hadi dola za marekani milioni 350.

‘’Vivutio vipo katika makundi mawili kwa hawa wawekezaji mahiri na ile maalumu kuna kamati ya Taifa ya uwekezaji ambayo mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, na ukiangalia mwezi machi mwaka huu tumetia saini makampuni takribani sita’’ Amebainisha Mnzava.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania –TIC kimeanzishwa kwa mujibu wa sheria sura ya thelathini na nane na iliundwa mwaka 1997 huku jukumu lake la msingi wa sheria hiyo ni kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini

0/Post a Comment/Comments