UPUNGUFU WA MVUA WASABABISHA SHIRIKA LA BIMA NIC KUTOA RAI KWA WAKULIMA NCHINI.



Afisa Bima kutoka Shirika la Bima la Taifa –NIC  Prosper Peter akizungumza jijini Dar es salaam
.........................

NA MUSSA KHALID

Wakulima nchini wametakiwa kuwekeza katika Bima za kilimo ili waweze kunufaika nayo na kuepukana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha upungufu wa mvua.

Hayo yameelezewa leo jijini Dar es salaam na Afisa Bima kutoka Shirika la Bima la Taifa –NIC Prosper Peter wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi kuhusu Shirika hilo linavyowasaidia wananchi na kukabiliana na changamoto inayotokana na upungufu wa mvua ambayo inasababisha hali ya ukame katika maeneo mbalimbali nchini.

Afisa Bima huyo amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima kufahamu aina mbalimbali za bima ambapo za mazao zimegawanyika katika aina mbili ikiwemo ya Bima ya Hali ya Hewa pamoja na Bima mseto.

‘Tumeamua kuanzisha Bima za Kilimo,mazao na uvuvi tangu Mwaka 2019 tumekuwa tukitoa huduma hiyo mpaka Sasa"amesema Peter

Peter amesema wataendelea kuhamasisha na kutoa elimu katika mikoa tofauti ili kuweza kuwasaidia wakulima wapate uelewa wa kufahamu matumizi sahihi ya bima hizo.

Hata hivyo Shirika la Bima la Taifa –NIC limesema kwa mujibu wa takwimu kwa wakulima wanaojiunga na Bima imekuwa ikiongezeka hivyo wengi wameendelea kunufaika katika shughuli zao za kilimo.

Ikumbukwe kuwa Oct,26 mwaka huu Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Tanzania –TMA kupitia Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka hiyo Dkt Hamza Kabelwa imetabiri uwepo wa upungufu wa Mvua za msimu kwa kipindi cha Novemba 2022 mpaka April 2023.

Alisema kuwa maeneo yanayotarajiwa kupata Mvua za chini ya wastani,upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama unaweza kujitokeza na kupelekea milipuko ya magojwa kama vile kipindupindu, homa ya matumbo na vikope.

0/Post a Comment/Comments