Na
Timotheo Mathayo, Dar es salaam.
Rais
Samia Suluhu Hassan ameagiza Taasisi na Idara za umma na binafsi zenye watu
wasiopungua 300 kutumia nishati safi kupikia chakula badala ya kutumia kuni au
mkaa.
Ametoa
agizo hilo leo Jumanne Novemba 01, 2022 wakati wafunguzi wa mjadala kuhusu
Nishati safi ya kupikia unaofanyika katika ukumbi wa mikutano ya kimataifa wa
Julias Nyerere.
Amemuagiza
Waziri wa Nishati, January Makamba kuhakikisha idara na taasisi zote za umma na
binafsi zenye mkusanyiko wa watu zaidi ya 300 kutumia Nishati safi kupika
chakula.
"Hili
agizo nataka lianze kutekelezwa mwaka 2023/2024. Mwaka huu wote wa 2022/2023
utumike kwa maandalizi ili Shule, Magereza, Majeshi na taasisi nyingine zenye
watu wengi zaidi wapike kwa kitumia nishati safi," amesema Rais Samia.
Pia
amewaagiza wakuu wa mikoa ya Pwani na Dar es salaam kufanya ukaguzi ili
kudhibiti na kukamata watu wanaoharibu vyanzo vinavyopeleka maji mto Ruvu ambao
ni chanzo kikuu cha maji katika mikoa hiyo.
"Kuna
watu wamechepusha maji na kuingiza katika mashamba yao na wengine wanaingiza
maji kwenye mabwawa ya kufugia samaki. Nawaagiza kaondoeni vizuizi vyote vya
maji katika eneo la mto Ruvu," amesema Rais Samia.
Mikoa
ya Pwani, Morogoro, Ruvuma, Tabora na Lindi imetajwa kuwa vinara wa kuharibu
mazingira kwa kukata misitu ovyo, jambo linalochangia kuleta athari za
kimazingira katika mikoa hiyo na mikoa jirani.
Awali
akimkaribisha Rais Samia kufungua
mjadala huo, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kupika sio adhabu,
hivyo sio vizuri watu kupika huku wakitokwa machozi kutokana na moshi wa kuni
au mkaa.
Amesema
watoto wa kike wapo katika hatari ya mbalimbali kutokana na wao kwenda porini
kutafuta kuni za kupikia au kuuza ili wapate kipato cha kaya.
Lengo la mjadala huo ni kutaka jamii iondokane na matumizi ya Nishati isiyo salama, kwa kuwa nishati hiyo ina athari kwa afya ya binadamu, lakini pia inachangia mabadiliko ya tabia nchi na pia imeelekezwa kufikia asilimia 80% ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2032.






Post a Comment