MAWAZIRI WAKUBALIANA KUZUIA UKATILI KWA WATOTO

 



Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Mawaziri watatu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Desemba 21, 2022 wamekutana Jijini Dar es Salaam kujadili kuhusu suala la ukatili kwa wanafunzi wa shule na vyuo na kuweka mikakati ya kupambana na ukatili huo.

Mawaziri hao, Mhe. George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naMhe. Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa pamoja wamekubaliana kushirikiana kulifanyia kazi suala la kuzuia ukatili dhidi ya watoto.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mkenda amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Kamishna wa Elimu ndio yenye jukumu kisheria la kutoa miongozo mbalimbali ya wanafunzi hivyo ina jukumu pia la kushiriki katika kuwalinda dhidi ya ukatili.

“Kikao hiki kitatusaidia kuongeza nguvu, badala ya kutumia Mwongozo wa Kamishna wa Elimu pekee ni vizuri akae na wataalamu kutoka Wizara nyingine husika ili kuangalia udhaifu upo kwenye miongozo au katika kuratibu utendaji na kisha kutolea taarifa,” amesema Waziri Mkenda.

Mkenda ameongeza kuwa Wizara ya Elimu inalo jukumu la kusimamia mpaka ngazi ya vyuo, hivyo mipango na mikakati itakayowekwa itaangalia ngazi hizo pia.

“Ni ukweli watoto wetu wanatumia muda mrefu katika shule na vyuo hivyo ni wajibu wetu kama walezi kuhakikisha huko kunakuwa mahali salama kwa watoto,” amesema Prof. Mkenda.

Kwa upande wake Mhe. Gwajima amesema kuwa ameshukuru kuungana katika mapambano dhidi ya ukatili, akitoa mfano mwaka 2021 takwimu zinaonesha jumla ya watoto 11,499 wamefanyiwa ukatili ikiwemo ubakaji, ulawiti na wengine kupata mimba za utotoni.

“Hao ni chini ya asilimia 15 ya walioripoti visa hivyo, ukatili huo ni pamoja na ubakaji, ulawiti na wengine kuishia kupata mimba za utotoni. Ukiangalia ukubwa wa tatizo na ukizingatia si wote wanaoripoti tumeona kuna ulazima wa kuangalia kwa pamoja wapi tuimarishe ili kukabiliana na tatizo hili,” amefafanua Dkt. Gwajima.

Ameongeza kuwa wazazi wanatakiwa washiriki kwa kiwango kikubwa kwenye suala hilo kwa kuwa takwimu zinaonesha asilimia 60 ya ukatili wa jinsia kwa watoto unafanyika majumbani ambapo kuna wazazi.

Kikao hicho kiliongozwa na Mhe. Simbachawene ambaye amesema kuwa Serikali imeipa umuhimu wa pekee suala hilo na hivyo kukubaliana kwa haraka sana kabla shule hazijafunguliwa kuwe na mikakati ya kuwalinda watoto itakayoshirikisha Wizara, Taasisi na makundi yote muhimu.

Mhe Simbachawene ameelekeza Makatibu Wakuu wa Wizara hizo Tatu wakiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kuhakikisha wataalamu wanaandaa mikakati ya muda mfupi na mrefu itakayojadiliwa na mawaziri na wadau.

“Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Elimu, OR – TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na makundi yote ikiwemo ya wazazi ni lazima kushirikiana ili tupate maoni na kila mmoja aone wajibu wake kuhusiana na suala hili la ukatili kwa watoto,” ameongeza Mhe. Simbachawene.

Aidha, Waziri Simbachawene ameagiza Mawaziri wote wanaohusika kukutana Januari 4, 2023 kupitia mikakati iliyowekwa na maoni yaliyotolewa na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kuridhiwa.

0/Post a Comment/Comments