Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa mkutano wake na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jorgesen. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, Kamishina Msaidizi wa Idara ya Mipango ya Kitaifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Treza Mtenga, Msaidizi wa Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. Alex Mwakisu na Afisa Dawati kutoka Idara ya Fedha za Nje, Bi. Devotha Lugenda.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Qatar)
.......................
Na Josephine Majura, (WFM) Doha Qatar
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa Denmark
imekubali kushirikiana na Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi
ambayo yamekua yakiathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Dkt.
Nchemba ameyasema hayo mjini Doha nchini Qatar, baada ya kukutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya
Tabianchi wa Serikali ya Kifalme ya Denmark, Mhe. Dan Jorgesen, kando ya
Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa nchi zinazoendelea
za kipato cha chini unaoendelea nchini humo.
Alisema nchi hizo mbili zimekubaliana kuzielekeza Taasisi zao
kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali hususani kukabiliana na
mabadiliko hayo ya tabia nchi ili kukuza uchumi.
“Licha ya makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huu, tumekua
na ushirikiano mzuri na Dernmark ambapo Serikali yetu hupokea fedha nyingi
kupitia Taasisi za Denmark ambazo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa mkutano kati ya nchi hizo mbili ni mwendelezo wa
mikutano mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika hivyo mazungumzo ya sasa ni
jitihada za kuendelea kuimarisha ushirikiano huo wa kimaendeleo katika sekta
mbalimbali.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar,
Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa Serikali ya Zanzibar imepata
manufaa makubwa katika sekta za kijamii ikiwemo afya, elimu na
miundombinu.
Alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla imeweka mikakati kabambe
ya kuhakikisha inatekeleza diplomasia ya kiuchumi na nchi mbalimbali ili
kuvutia uwekezaji na kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo mikutano inayoendelea
na nchi nyingine ni miongoni mwa jitihada za kufanikisha azma hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za
Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jorgesen, ameipongeza Tanzania kwa
kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo.
Mhe. Jorgesen amesema kuwa pamoja na upya wa Serikali yake
iliyopo madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa Novemba 2022, Serikali ya mseto ya
Denmark itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali
za kiuchumi na kijamii.
“Mabadiliko
ya Tabianchi ni masuala ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele na kila mmoja wetu
kutokana na athari zinazoendelea kujitokeza kutokana na changamoto hiyo”,
alisema Mhe. Jorgesen.
Aidha, Mhe. Jorgesen alisema Serikali yake inayoongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Mette Frederiksen, anao ufahamu mkubwa kuhusu siasa za Bara la Afrika hivyo itasaidia kuongeza ushirikiano kati ya Denmark na Tanzania.



Post a Comment