UKOSEFU WA MVUA WAIBUA USHIRIKINA B'MULO

 



*********************************************

Na Daniel Limbe,Biharamulo

UKOSEFU wa mvua kwenye kata ya Kalenge wilayani Biharamulo mkoani Kagera, umedaiwa kutishia maisha ya watu kutokana na baadhi yao kutuhumiana kwa ushirikina.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wananchi kutumia gharama kubwa kulima mazao yao kisha kukauka kutokana na uhaba wa mvua ambazo zimekuwa zikinyesha kwenye baadhi ya mikoa hapa nchini.

Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method,amesema hayo leo Machi 6 kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmaahauri hiyo wakati akiwasilisha taarifa za kata yake licha ya kudai kwamba elimu imeendelea kutolewa.

"Miongoni mwa changamoto zilizopo kwenye kata yangu ni pamoja na matishio ya uvunjifu wa amani kutokana na baadhi ya wananchi kutuhumiwa kuzuia mvua kunyesha...hata hivyo tumefanikiwa kuzibiti uvunjifu huo wa amani kwa kuendelea kuwaelimisha wananchi kutojichukulia sheria mkononi"amesema Method.

Kadhalika baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijinadi kuwa wanao uwezo wa kuita mvua ili inyeshe baada ya kupewa fedha,pia wamekuwa wakichangia sana tishio la wananchi kutaka kujichukulia sheria mkononi.

Mbali na hilo,Method amelia na matokeo mabovu ya wananfunzi wa shule za msingi na sekondari huku akidai baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia watoto wao kufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba.

Kauli hiyo,ikaungwa mkono na Kaimu Ofisa elimu shule za msingi wilayani humo, Hauson Revelian, ambaye amekiri kuwepo kwa tabia ya baadhi ya wazazi kuwarubuni watoto wao kutofanya vizuri ili wasichagukiwe kujiunga na shule za sekondari.

Kutokana na hali hiyo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushau,akalazimika kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwahamisha walimu wote ambao shule zao zimekuwa na matokeo mabovu ya msingi na sekondari.

"Bahati nzuri kwenye kata ya Kalenge nimefika mwenyewe na kuzungumza na wazazi...chanzo kikubwa walichosema kinasababisha kuwazuia watoto wao kufanya vizuri kwenye mitihani yao ni pamoja na matokeo mabovu ya watoto wao waliotangulia kuingia sekondari...kwani inawanyima mwamko wa kuendelea kuwasomesha wengine waliopo nyumbani"amesema Rushau.

Hata hivyo amesema aslimia 36 ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi kwenye kata hiyo haukubariki na hauwezi kufumbiwa macho kwa kuwa unatia aibu kwenye wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla.


                          Mwisho.

0/Post a Comment/Comments