Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji na Watumishi wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA) kuzingatia maslahi ya Watanzania na maslahi ya nchi katika kazi zao za Udhibiti wa Huduma za Nishati
na Maji ili Watanzania wapate
huduma bora na kwa unafuu mkubwa.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifungua Kikao
cha Baraza la Pili la Wafanyakazi
wa Mamlaka hiyo kilichofanyika tarehe 8 Novemba, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali
akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE
Taifa, Rugemalira Rutatinwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa.
“Tambueni kuwa Taifa lina mategemeno makubwa na
ninyi, hivyo fanyeni kazi zenu kwa
weledi na ubunifu mkubwa unaoendana na kasi ya teknolojia na maendeleo ya dunia; kanuni na miongozo
yenu mnayotumia katika utekelezaji
wa majukumu iundwe katika mifumo rafiki kulingana na hali iliyopo ili ilenge kuleta matokeo chanya kwa
ustawi wa Taifa na hivyo
Watanzania waendelee kupata huduma bora na kwa gharama stahiki.” Amesema Dkt. Biteko
Pia amewataka Watumishi wa EWURA kuweka mkazo
kwenye kudhibiti vitendo vya
urasimu na rushwa mahali pa kazi, kutoangalia maslahi binafsi wakati wa kutenda kazi ili kuepusha kuwaumiza
Watanzania walio wengi, na ametoa
wito kwa wafanyakazi hao kumkemea mtu yeyote anayeonekana kuwa na vitendo vya rushwa na ubinafsi katika eneo la
kazi.
Vilevile, amewasisitiza Wafanyakazi wa EWURA
kuwajibika ipasavyo katika
kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha kuwa Watoa Huduma wanafanya ushindani wenye tija na ufanisi wa kiuchumi,
kulinda maslahi ya Walaji na
mitaji ya kifedha ya Watoa Huduma pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ikiwemo ya watu
wanaoishi vijijini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu
ameipongeza EWURA kwa kupitia upya
gharama za uagizaji wa mafuta ambazo amesema kuwa, awali zilikuwa
kubwa na zilikuwa zikipelekea athari mbalimbali
ikiwemo kuongezeka kwa gharama
katika Sekta ya Usafirishaji na Uzalishaji.
“Gharama hizi za uagizaji mafuta zilikuwa kubwa
mno huku kukiwa hakuna
sababu ya kuwa kubwa kwa kiasi hicho, niliwapa
maelekezo mkazitazame
upya, nashukuru mmeziangalia na ninafurahi kwamba
zimeshuka na hivyo
kupunguza makali kwa watumiaji." Amesema Dkt.
Biteko.
Vilevile Naibu Waziri Mkuu ameiagiza TUGHE-
Taifa kueleza juhudi zinazofanywa
na Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu masuala ya Wafanyakazi akitolea mfano upandishwaji madaraja wa
mseleleko kwa watumishi ambao
hawajapanda madaraja kwa muda mrefu.
Amewataka pia kuwashirikisha wanachama wao ili
kuisaidia Serikali katika kupeleka maendeleo
kwa wananchi na pia kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu wake kwa Wafanyakazi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James
Andilile alisema kuwa, Taasisi
hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi lengo likiwa ni kuhakikisha Huduma za Nishati na Maji zinapatikana
kwa uhakika, kwa kutosha, kwa
uendelevu na kwa gharama ambazo wananchi wanazidumu.
Alimshukuru, Dkt. Biteko kwa kutoa ushirikiano
mkubwa kwa Taasisi hiyo na
miongozo anayotoa ambayo inafanya EWURA iendelee kuboresha utendaji
wake katika kuhudumia Watanzania.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa EWURA
kinachoendelea jijini Dodoma
kimelenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo
utekelezaji wa Bajeti ya
EWURA kwa mwaka 2022/2023 na Taarifa ya Ukaguzi wa
Hesabu za EWURA za
mwaka 2022/23
Post a Comment