*****************
Shirika
la Masoko ya Kariakoo (KMC) limesema mradi wa ujenzi wa ukarabati wa Soko la
Kariakoo umefikia asilimia 93 ili kukamilishwa
tayari kuwarejesha wafanyabiashara kwenye soko hilo, ambapo litafanyakazi
kwa saa 24.
Kwa
mujibu wa uongozi wa soko hilo hadi sasa hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa
ikiwemo utambuzi na uhakiki wa waliokuwa wafanyabiashara kabla ya janga la
moto.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Mkuu wa
Shirika la masoko ya Kariakoo (KMC), Sigsibert Valentine, amesema kazi nyingine
inayoendelea ni kupanga biashara kulingana na eneo husika pamoja na kufuatilia
madeni ya waliokuwa wafanyabiashara wa soko la kariakoo.
Valentine
amezitaja faida mbalimbali ambazo zitapatikana pale mradi huo utakapokamilika
kuwa ni kuongezeka kwa nafasi za biashara kufikia 3,500, ajira zisizo za moja
kwa moja zisizopungua 4,000, kuboresha mandhari ya jiji la Dar es Salaam ambalo
ni kitovu cha biashara nchini.
Fursa ni nyingine ni wafanyabiashara kuwa na
uwezo wa kufanya biashara kwa masaa 24, mapato ya Serikali kuongezeka maradufu
kupitia tozo, ada na ushuru, lakini pia kuendeleza historia ya soko la Kariakoo
kama kivutio cha utalii”
Kuhusu muda rasmi wa kurejea wafanyabiashara
sokoni Kariakoo, Valentine amesema taarifa rasmi itatolewa na Serikali mara
baada ya kukamilika kwa hatua za mwisho za mradi wa ujenzi.
Kuhusu madeni ya wafanyabiashara, Valentine
amesema takwimu za shirika la masoko ya kariakoo zinaonesha kuwa sh.
497,773,019.00 madeni ambayo walilimbikiza kwa muda mrefu ambapo madeni hayo
yanapaswa kuwa yamelipwa na wafanyabiashara kabla ya kurejea sokoni ili wapate
nafasi ya kusajiliwa na mfumo.
Amesema hadi sasa kiasi cha sh. 15,830,977.71
sawa na asilimia 3 ya deni linalodaiwa kimekusanywa hadi Aprili 2024
Amewataka wafanyabiashara kutimiza wajibu wao
wa kisheria wa kulipa deni alilokuwa amelimbikiza kabla ya kusitisha shughuli
za biashara Julai 10, 2021 kwenye soko hilo.
“Kwa taarifa hii, Shirika la Masoko ya
Kariakoo linapenda kuwakumbusha wafanyabiashara kutumia kipindi hiki kifupi
kilichobaki kabla ya ufunguzi rasmi wa soko kukamilisha ulipaji madeni yao
hatua itakayoondosha malalamiko na usumbufu wakati wa kuomba nafasi,”amesema.
Mbali na hayo, Valentine amesema kutokana na
maboresho yanayofanyika katika uendeshaji wa biashara katika soko jipya la
Kariakoo na maagizo ya Serikali kutumia mifumo ya kielektoniki ili kuleta tija,
Shirika litatumia mfumo wa kielektoniki wa TAUSI kutangaza maeneo ya biashara
na kukusanya mapato.
“Shirika halitaruhusu mfanyabiashara mwenye
deni la awali kupata umiliki wa eneo la kufanya biashara katika Soko la
Kariakoo.”
Valentine amesema Serikali inaendelea
kushirikiana na wadau wote wa soko la Kariakoo wakiwemo wafanyabiashara,
Mamlaka za usimamizi na udhibiti wa majanga pamoja na kodi kuhakikisha
soko litakapoanza kazi linakuwa na viwango vya kimataifa vya usalama ili
kuleta ufanisi na tija katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Post a Comment