**************
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu na mchango wa utafiti wa
kisayansi katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisayansi zinazochangia kuchochea
maendeleo ya nchi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Mei 14, 2024 jijini Dar es
salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Philip Mpango katika ufunguzi wa Mkutano wa 32 wa Masuala ya Utafiti
wa Kisayansi ulioandaliwa na Taasisi ya
Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
‘‘Serikali
inayoongozwa na Rais Samia inaamini katika tafiti za kisayansi na inaamini pia
kuwa hakuna maendeleo bila utafiti na hivyo ili kupata mafanikio ni lazima
tufanye utafiti’’, amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza ‘‘Kama mnavyofahamu kupata maendeleo ya mahali
popote ili matokeo yaonekane lazima kuwe na utafiti wa kisayansi na uweze kuwa
na matumizi mazuri ya rasilimali kwa hivyo maendeleo yoyote bila utafiti
yatakuwa ni maendeleo ya kubahatisha, na kama ni ya kubahatisha kutakuwa na
kukosea kungwi matokeo yake kutakuwa na matumizi ya rasilimali nyingi zaidi
kabla ya kupata jibu sahihi jambo ambalo lingeepukika, hivyo wataalamu hawa
wako hapa kujadili tafiti mbalimbali
katika sekta ya afya mfano chanjo’’.
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa
kipaumbele kwa sekta ya afya na itaendelea kuunga mkono tafiti za kisayansi
huku akiziasa taasisi za utafiti kushirikiana katika tafiti kwa lengo la
kutatua changamoto mbalimbali ili kuchangia maendeleo ya nchi.
Sambamba na hilo, Dkt. Biteko amesema Serikali imewekeza vya kutosha kwenye utafiti katika
sekta ya afya ili kuwa na ugunduzi wa ndani ya nchi
akiongeza kuwa pamoja umuhimu wa watafiti kutoka nje kuna umuhimu wa kuwa wagunduzi wa
ndani.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel
amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kutoa kipaumbele katika
masuala ya utafiti kwa lengo la kuwajengea uwezo watafiti wa ndani ya nchi ili
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohitaji utafiti wa kisayansi mara
zitakapotokea.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Taifa ya
Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka
Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa na
ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi kupitia tafiti zake mbalimbali inazofanya
akitolea mfano ugunduzi wa dozi moja ya chanjo ya mlango wa kizazi uliofanywa
na NIMR mkoani Mwanza.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya
Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiendesha
makongamano kwa kushirikiana na wadau ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika
kuboresha sera za afya pamoja na kufanya maamuzi yanayosaidia kuboresha sekta
hiyo nchini.
Awali, Dkt. Biteko ametembelea mabanda ya vifaa vya maabara
vya kupima magonjwa mbalimbali ikwemo kifua kikuu, malaria na tafiti za dawa za
asili.

.jpeg)


Post a Comment