MATUMIZI YA NISHATI SAFI KUPIKIA YANAVYOWEZA KUNUSURU BINADAMU KUTOWEKA


Mwonekano wa mitungi ya gesi ya kupikia
*****

Na Daniel Limbe,Torch media

"Dunia yetu haiwezi kuwa salama kama mazingira hayako salama, hewa tunayovuta haiwezi kuwa salama kama mazingira yetu hayako salama."

Nukuu hii inalenga kuonyesha umuhimu wa kutunza Mazingira tunayoishi kwa manufaa ya watu na viumbe hai wengine duniani.

Ni muhimu tutambue kuwa Mazingira yakiangamia na binadamu tutaangamia, Mazingira yakipotea na binadamu tutapotea, na iwapo nchi itakuwa jangwa tutalima wapi.

Hata hivyo huu siyo wakati wa kulaumiana kuwa nani katufikisha hapa kwa kukata miti ovyo,bali ni muda wa kuchukua hatua kwa kukubali mabadiliko chanya kwa kuwa bado inawezekana.

Ipo Methali ya Kituruki inayosema "Haijalishi umeenda umbali kiasi gani kama umepotea njia, rudi nyuma," ni wakati mwingine mzuri wa kurejea katika utunzaji mazingira kwa kupanda miti, kuitunza na kuilinda kwa wivu mkubwa.

Kwa kuzingatia utangulizi huo ni wazi kuwa, serikali yetu bado inapaswa kusimama kidete katika suala zima la matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kudhibiti uharibifu mkubwa wa mazingira unaotishia kutokea jangwa siku za usoni.

Tishio hilo linatokana na kasi kubwa ya watu kukata miti ovyo kwa lengo la kuandaa kuni,kuchoma mkaa,kupasua mbao,kuweka nguzo kwenye machimbo ya dhahabu (matimba) na kilimo cha kuhama hama hasa vijijini.

 *MKAKATI WA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA* 

Kwa ujumla kama nilivyojaribu kusema hapo juu,huu siyo muda wa kulaumiana wala kushikana mashati kuwa nani katufikisha hapa tulipo ispokuwa wimbo wetu unapaswa kuwa nishati safi ya kupikia ni hitaji la kila siku katika maisha ya watanzania wote.

Ingawa bado kuna ukweli mchungu kwamba, pamoja na uhitaji huo sheria zetu hazisimamiwi ipasavyo kulingana na uharibifu mkubwa wa Mazingira unaoendelea nchini kutokana na baadhi ya watumishi wa Umma kuendekeza maslahi binafsi.

Zipo sheria zetu nzuri, ikiwemo ya Sheria ya Usimamizi wa mazingira sura 191 kifungu cha 58 (2) kinaelekeza kuhusu hifadhi ya mazingira na ulinzi wa milima,vilima na miinuko na Sera ya Misitu ya mwaka 1998 imeelekeza utaratibu wa kutunza na kuhifadhi.

Vile vile Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Misitu Sura 323, zimeweka utaratibu wa kisheria kudhibiti uharibifu wa mazingira hususani ukataji miti holela katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya milima na miinuko.

Hata hivyo zipo jitihada kubwa za serikali zinazopaswa kupongezwa katika suala hili ikiwemo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan,kupiga marufuku taasisi zote zenye idadi ya kuanzia watu 100 kuacha kutumia kuni katika kuandaa chakula badala yake zitumie nishati safi ya kupikia ikiwemo, gesi, umeme na makaa ya mawe.

Msingi huo umekolezwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na Jeshi la magereza, ambalo limekuwa likitumia kuni kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwake hapa nchini.

Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoa wa Geita,ACP Jonam Mwakasagule, amesema nia ya serikali kuzitaka taasisi za umma kutumia nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono na jamii nzima.

"Sisi kama Jeshi la Magereza tulikuwa tunapata shida sana wakati tunatumia kuni kupika na tulikuwa tunapotezea muda mwingi porini kutafuta nishati hiyo,"

"Wakati mwingine tulikuwa katika hatari kubwa ya usalama wa maisha yetu kutokana na wanyama pori wakali kama vile nyoka na wanyama wengine" amesema ACP Mwakasagule.

Amesema kuwa matumizi ya nishati safi katika jeshi hilo sasa yamepewa kipaumbe mkoani humo ili kujenga afya bora na kupunguza magonjwa ya macho pamoja na kifua kutokana na matumizi ya kuni wakati wa kupika chakula.

 *UJIO WA KIWANDA CHA MKAA MBADALA* 

Kubadilisha fikra za baadhi ya watu katika matumizi ya mkaa na kuni siyo jambo jepesi sana,ispokuwa wanahitajika kuona njia mbadala na iliyorafiki kwao ili kukimbilia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kutokana na ukweli huo,Wakala wa Nishati Vijijini(Rea) kwa kushirikiana na Shirika la Madini nchini(Stamico) wanakuja na mpango wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala mkoani Geita ili kuokoa mazingira na afya za watu.

Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini,Ahmed Chinemba, amesema serikali ipo kwenye maandalizi ya kujenga kiwanda hicho kwaajili ya kuongeza ufanisi wa jamii kutumia nishati mbadala hasa vijijini.

Hatua hiyo itasaidia kunusuru ukataji wa miti ovyo na badala yake jamii itapaswa kuendelea kutunza Mazingira ili yawe endelevu kwa sasa na vizazi vijavyo.

"Tukumbuke kuwa maerekezo ya Rais ni kuwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ziachane na matumizi ya kuni na mkaa, na kwamba zinapaswa kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa, “

"Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia katika mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024 - 2034)."amesema Chinemba.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadilifu nchini,Mhandisi Innocent Luoga, amesema Tanzania ndiyo nchi kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa nchi za Afrika mashariki kutokana na sera na miongozo iliyojiwekea ili kufikia malengo.

"Kwa Tanzania safari ya nishati safi ya kupikia tuliianza rasmi mwaka 2022 ambapo Rais Dkt. Samia alianzisha mjadala wa nishati hii kupitia wadau mbalimbali na kutoa maelekezo ya utekelezaji ikiwemo ya kuanzishwa mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao ulizinduliwa mwaka 2024 ukiwa unaelekeza kuwa aslimia 80 ya watanzania wanapaswa kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034."

Amesema ii kufikia malengo ya mpango huo,serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo kugawa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku,kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na kusambaza gesi asilia kwa njia ya bomba hasa kwa baadhi ya mikoa ya Lindi,Mtwara na Dar es salaam.

"Hatua nyingine ni kuweka unafuu wa Kodi kwa baadhi ya vifaa vya nishati safi ya kupikia vinavyoingia nchini pamoja na kupitia Sheria,kanuni na Sera ili kuangalia maeneo yatakayo rahisisha upatikanaji wa nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Luoga, takribani watu bilioni 2.1 duniani hawatumii nishati safi ya kupikia huku nchi za ukanda wa Jangwa la Sahara zikiwa ni watu milioni 990 wasio tumia nishati hiyo safi.

Kadhalika kwa Tanzania watu wanaotumia nishati safi ya kupikia ni takribani aslimia 16 pekee huku malengo ya serikali yakiwa ni wananchi wote kutumia nishati hiyo muhimu.

 *MAKAMU WA RAIS* 

Akiwa kwenye mkutano maalum wa viongozi, wataalamu na wadau wa mazingira kuhusu hali ya mazingira nchini, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mipango, anasema Tanzania inalia na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi na kwamba hali hiyo inahatarisha uhai wa viumbe vyote ikiwemo sisi wanadamu.

Amesema taarifa ya nne ya mazingira ya mwaka 2024 inaonyesha hali ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini hairidhishi.

"Nchi yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali za mazingira ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na tabia ya watu kukata miti ovyo na uharibifu wa misitu ambapo takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la uharibifu wa misitu kutoka hekta 372,816 kwa mwaka 2019 hadi kufikia 469,420 kwa mwaka 2023." amesema Dkt. Mpango.

Kwa mujibu wa Dkt. Mpango,wastani wa hekta 24,151 zinapotea kila mwaka na uharibifu huo unachangiwa kwa sehemu kubwa na shughuli za kibinadamu zisizo kuwa endelevu ikiwemo utegemezi mkubwa wa nishati ya kuni na mkaa.

"Katika matumizi ya nishati chafu,takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,zinaonyesha kuwa aslimia 82 ya nishati inayotumika kwa ajili ya kupikia inatokana na kuni na mkaa" amesema Dkt. Mpango.

 *SHIRIKA LA UNDP* 

Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Shigeki Komatsubara, anaipongeza Tanzania kwa kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia kupitia jitihada mbalimbali huku akidai kuwa kielelezo kikuu ni uwepo wa Mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ambao ni Dira katika kufikia lengo la aslimia 80 ya watanzania wanaopaswa kutumia nishati hiyo.

"Suala la nishati safi ya kupikia siyo la Tanzania pekee bali ni la dunia nzima,hivyo ushirikiano unahitajika ili kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa duniani pote kwa kuwa ni suala linalohusu usalama wa afya na mazingira ya mwanadamu na viumbe wengine" amesema Komatsubara.

Hali kadhalika anazipongeza nchi za Afrika mashariki kwa kuendelea kusukuma mbele ajenda ya matumizi ya nishati safi inayolenga katika matumizi ya teknolojia safi, bora na endelevu kwa maisha ya sasa na baadaye.

 *NINI KIFANYIKE* 

Baadhi ya wadau wa mazingira akiwemo Hadija Omari na Rethisia Kaswahili wanaishauri serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma ili watu watambue umuhimu wa kuhifadhi misitu na kupanda miti.

Wazee wa mila washirikishwe katika vikao mbalimbali hasa vijijini ili kutoa uzoefu wao katika kuhifadhi mazingira.

Wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) waoteshe miche ya kutosha na kuigawa kwa watu ili kila mwananchi ashiriki katika kupanda na kutunza miche isiyopungua 10.

"Sheria zilizopo zisimamiwe kikamilifu na zile ambazo zinakinzana na uhifadhi wa mazingira zifumuliwe na kufanyiwa maboresho mapya kulingana na hali halisi wa sasa,"

"Serikali iweke ruzuku kwenye nishati safi ya kupikia ili ipatikane kwa wepesi na gharama nafuu hasa kwa wananchi waishio vijijini, wachimba Madini watumie vyuma badala ya matimba na vijiji viheshimu matumizi bora ya ardhi ili kudhibiti wakulima kuhamia maeneo mengine na kukata miti ovyo." anahitimisha Kaswahili.

Ipo nukuu ya Chinese Proverb aliwahi kusema “Muda mzuri wa kupanda mti ni miaka 20 iliyopita, Lakini muda mwingine mzuri wa pili ni sasa.”

                      Mwisho

 

0/Post a Comment/Comments