,%20Ushirikiano%20huu%20unalenga%20kuunda%20mazingira%20jumuishi%20ya%20kidijitali%20kwa%20zaidi%20ya%20biashara%202,000%20zitakazofanyika%20%20(7).jpg)
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Kampuni ya mawasiliano ya Yas imeingia makubaliano ya kimkakati na East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC), lengo kuu likiwa ni kuimarisha mazingira jumuishi ya kidijitali kwa zaidi ya biashara 2,000 zitakazohudumiwa ndani ya jengo jipya la kibiashara la EACLC lililopo Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Kupitia makubaliano hayo, Yas imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya intaneti ya fiber optic yenye kasi ya hali ya juu, ili kuwezesha mawasiliano ya uhakika na matumizi ya zana mbalimbali za kidijitali kwa wafanyabiashara wa jengo hilo.
Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, mwakilishi wa kampuni ya Yas alisema, “Tunalenga kuwapa wafanyabiashara mazingira bora yatakayowawezesha kufanikisha malengo yao kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kuhakikisha biashara nchini zinaendeshwa kwa ufanisi zaidi.”
Mbali na huduma za intaneti, Yas pia itatoa huduma za Mixx, mfumo wa malipo ya kidijitali unaowawezesha wateja na wafanyabiashara kufanya miamala mbalimbali moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi, hivyo kurahisisha shughuli za kila siku.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mpango huu unalenga kuwafikia wajasiriamali wadogo kwa wakubwa, huku ukilenga kuongeza usalama wa miamala, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi wa biashara kwa Watanzania wote.
“Tunafungua ukurasa mpya katika kufanya biashara kuwa rahisi, salama na ya kisasa kwa kila Mtanzania, na huu ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa kwenye sekta ya biashara nchini,” ilielezwa katika taarifa ya pamoja ya Yas na EACLC.
Jengo la EACLC linatarajiwa kuwa kitovu kikuu cha biashara na huduma jijini Dar es Salaam, na kupitia ushirikiano huu, linapewa msukumo wa kuwa mfano wa matumizi bora ya teknolojia katika maendeleo ya kiuchumi.
Post a Comment