MAFANIKIO YA GEREZA LA PAWAGA YASHANGAZA WENGI TANZANIA

......

Na Carlos Claudio, Iringa.

Jeshi la Magereza nchini limetoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wafungwa wanaomaliza vifungo vyao, na badala yake kuwakaribisha na kuwashirikisha katika shughuli za kiuchumi na kijamii ili waweze kuchangia maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Gereza la Pawaga mkoani Iringa, SSP Jawadu Abdallah, aliyesisitiza kuwa wafungwa hupatiwa mafunzo mbalimbali ya ujuzi wakiwa gerezani, hatua inayowaandaa kuwa raia wema, wenye nidhamu na uwezo wa kujitegemea wanaporejea uraiani.

Amesema mapokezi mazuri kwa wafungwa wanaotoka gerezani ni sehemu muhimu ya kufanikisha juhudi za serikali katika utekelezaji wa miongozo ya urekebu, ambayo inalenga kuwabadilisha na kuwajenga upya wafungwa ili wawe na mchango chanya kwa jamii.

Katika hatua nyingine, Gereza la Pawaga limeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika uzalishaji wa chakula, hasa mpunga kupitia kilimo cha umwagiliaji. 

Gereza hilo limefanikiwa kuzalisha kiasi kikubwa cha mpunga kilichokidhi mahitaji ya mikoa 11 nchini, huku pia likiendeleza miradi ya ufugaji wa ng’ombe na mbuzi.

Akizungumzia mkakati wa gereza hilo, SSP Abdallah alisema lengo kuu ni kujitosheleza kwa chakula kwa kutumia ipasavyo hekari 270 walizopatiwa. 

Kwa msimu wa kilimo wa 2024/2025, walilima hekari 200 na kuvuna gunia 3,808 za mpunga ambazo zilisambazwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mara, Shinyanga, Singida, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Ruvuma na Mtwara.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Magereza na Bwana Shamba wa Gereza la Pawaga, Yusuph Kuchepa, alisema uzalishaji huo umewezesha kusaidia mikoa hiyo kujitosheleza kwa chakula kwa kipindi cha mwaka mzima.

Aidha, Mkaguzi wa Magereza Shaban Kibari, ambaye ni mtaalam wa mifugo, alieleza kuwa wafungwa hushirikishwa katika shughuli za ufugaji chini ya usimamizi wa askari, ambapo hupata mafunzo ya kina kuhusu utunzaji wa mifugo ikiwemo matibabu, ukamuaji, malezi ya ndama na mbinu bora za ufugaji.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wafungwa wanapotoka gerezani wanakuwa na ujuzi wa kujiajiri na kuwa mfano bora katika jamii.

Katika ushuhuda wa mafanikio ya mfumo huo wa urekebu, Ambrose Msakwa, mkazi wa Pawaga ambaye aliwahi kutumikia kifungo gerezani hapo, ameibuka kuwa kiongozi anayeaminika katika jamii baada ya kuchaguliwa kusimamia skimu ya umwagiliaji ya Mkombozi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 56.

Msakwa alisema licha ya changamoto alizokutana nazo baada ya kutoka gerezani, ameweza kurejea katika maisha ya kawaida na kuaminiwa na wananchi, hali inayothibitisha kuwa wafungwa wanaweza kubadilika na kuwa na mchango mkubwa kwa jamii.

Alisisitiza umuhimu wa jamii kuwaunga mkono na kuwapa nafasi watu waliotumikia vifungo vyao, akieleza kuwa nao ni sehemu ya jamii na wana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Aidha, aliipongeza serikali kwa kuendelea kuimarisha mfumo wa urekebu magerezani, akisema unawasaidia wafungwa kupata ujuzi na maarifa muhimu yanayowawezesha kujitegemea wanaporejea uraiani.







 

0/Post a Comment/Comments