.....
Na Carlos Claudio, Mbeya.
Mfumo wa magereza nchini umeendelea kubadilika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na ilivyokuwa kipindi cha ukoloni, ambapo wafungwa walikuwa wanapelekwa gerezani kwa ajili ya mateso badala ya kurekebishwa na kuandaliwa kurejea katika jamii wakiwa na mchango chanya.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya, Mkuu wa Magereza Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Raymond Mwampashe, amesema kuwa zamani mfumo wa magereza ulikuwa ukilenga zaidi adhabu na kulazimisha utiifu kwa matakwa ya wakoloni, bila kuzingatia mustakabali wa mfungwa baada ya kumaliza kifungo chake.
Amesema tofauti na ilivyokuwa hapo awali, hivi sasa mfumo wa magereza unalenga kumjenga mfungwa ili anapotoka awe amebadilika na kuwa na ujuzi utakaomwezesha kujitegemea katika maisha ya kila siku.
“Leo hii tunahakikisha mfungwa anapoingia gerezani hatoki kama alivyoingia. Lazima atoke akiwa na maarifa au ujuzi utakaomsaidia katika maisha yake ya baadaye,” amesema Mwampashe.
Ameeleza kuwa katika utekelezaji wa hilo, magereza yameanzisha programu mbalimbali za urekebu zikiwemo mafunzo ya ufundi kama useremala, uchomeleaji, ufundi bomba pamoja na shughuli za uzalishaji kama kilimo, mifugo na ufyatuaji wa matofali.
Aidha, amesema kuwa askari na maafisa wa magereza wanaendelea kupewa mafunzo maalum kupitia mitaala mipya inayotolewa katika vyuo vya magereza ikiwemo Chuo cha Kiwira, ili kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa kushughulikia wafungwa kwa mtazamo wa urekebu badala ya adhabu pekee.
Mwampashe amesema kuwa mfungwa anafundishwa kuwa mtaji wake mkubwa ni ujuzi pamoja na uaminifu, akibainisha kuwa bila uaminifu, hata ujuzi alionao hautakuwa na manufaa yoyote.
“Tunawaambia wafungwa kuwa hata kama hawana mtaji wa fedha, ujuzi wao unaweza kuwa mtaji tosha. Lakini uaminifu ndio msingi wa kila kitu,” ameongeza.
Pia ameeleza kuwa juhudi hizo zinaendana na maelekezo ya uongozi wa juu wa nchi chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, pamoja na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa kuboresha mfumo wa haki nchini.
Kwa mujibu wa Mwampashe, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafungwa wanaoingia magerezani hukosa ujuzi wowote wa kujitegemea, hali inayochangia baadhi yao kujikuta wakirejea katika makosa baada ya kutoka gerezani.
Amesema kupitia maboresho ya sasa, serikali inalenga kuhakikisha wafungwa wanapata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kurudia makosa na kuchangia maendeleo ya taifa.
Mwisho, ametoa wito kwa jamii kuwapokea na kuwapa fursa wafungwa wanaomaliza vifungo vyao ili waweze kutumia ujuzi walioupata gerezani kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.








Post a Comment