MIRADI YA MAGEREZA YAIBUA FURSA ZA UJASIRIAMALI

.................

Na Carlos Claudio, Mbeya.

Mkuu wa Gereza la Ruanda mkoani Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Magereza Christopher Fungo, amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na teknolojia ya kisasa ya uendeshaji wa kesi yameleta mapinduzi makubwa katika uendeshaji wa magereza na ustawi wa wafungwa.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea gereza hilo kujionea miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza, Fungo alisema kuwa gereza la Ruanda limeanza kutumia nishati safi ikiwemo makaa ya mawe mbadala na gesi, hatua ambayo imeondoa changamoto zilizokuwepo hapo awali.

Alieleza kuwa matumizi ya kuni yalikuwa yakisababisha upotevu mkubwa wa muda na fedha, pamoja na kuhatarisha usalama wa wafungwa waliokuwa wakipelekwa porini kukusanya kuni.

“Kwa sasa hali imebadilika kabisa. Tunapika kwa haraka zaidi, tunaokoa gharama, lakini muhimu zaidi tunalinda afya za wafungwa wetu,” alisema Fungo.

Katika hatua nyingine, alisema serikali imeboresha mfumo wa uendeshaji wa kesi kwa kuanzisha mahakama za mtandao, jambo linalopunguza gharama za kusafirisha wafungwa kwenda mahakamani.

Alifafanua kuwa baadhi ya kesi sasa zinaendeshwa kwa njia ya mtandao, huku zingine zikiendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Mbeya Mjini na Mahakama ya Wilaya ya Chunya kwa kutumia usafiri wa mabasi ya kisasa yaliyotolewa na serikali.

Aidha, Fungo alibainisha kuwa Jeshi la Magereza linaendelea kuimarisha dhana ya urekebishaji wa wafungwa kupitia hatua nne muhimu, kuanzia mapokezi yao wanapotoka mahakamani hadi kipindi cha utekelezaji wa adhabu na mafunzo ya stadi mbalimbali.

“Tunawapokea wafungwa kwa utu na upendo, tunawaeleza haki zao za msingi na kuwajenga kisaikolojia ili waone bado ni sehemu ya jamii,” alieleza.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha kutumikia adhabu, wafungwa hushirikishwa katika shughuli za uzalishaji mali na mafunzo ya ufundi stadi ikiwemo kilimo, ufyatuaji wa matofali, pamoja na kazi za mikono kwa upande wa wanawake kama ushonaji wa masweta, vitambaa na bidhaa za mapambo.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Magereza, Gilbert Harmon, akizungumzia mradi wa utengenezaji sabuni unaoendeshwa na Shirika la Magereza, alisema miradi hiyo inalenga kubadili fikra za wafungwa kutoka dhana ya adhabu kwenda urekebishaji na uzalishaji.

“Tunaangalia uwezo na mawazo ya kila mfungwa, kisha tunamjenga upya ili aweze kujitegemea na kuwa raia mwema anaporudi kwenye jamii,” alisema Gilbert.

Aidha, alitoa wito kwa jamii kuacha kuwanyanyapaa wafungwa wanaomaliza vifungo vyao, badala yake iwakubali na kuwapa nafasi ya kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

“Tunatumia muda mwingi kuwafundisha na kuwajenga. Wanapotoka wanakuwa na maarifa na ujuzi, hivyo jamii inapaswa kuwapokea kama watu waliobadilika na tayari kuchangia maendeleo,” alisisitiza.

Hatua hizi zinaonesha juhudi za serikali katika kuboresha mfumo wa magereza nchini kwa kuzingatia zaidi urekebishaji, utu na maendeleo ya wafungwa badala ya adhabu pekee.







 

0/Post a Comment/Comments