WRRB YARIDHISHWA NA USIMAMIZI WA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA MIKOANI

 

Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeanza rasmi utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ya kuimarisha usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake zinatatuliwa bila kurudi kwenye biashara holela ya mazao.

Akitoa taarifa baada ya kutembelea mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Morogoro na Iringa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo hayo aliyoyatoa kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi hiyo Mei 19, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema katika ziara hiyo amekutana na viongozi wa mikoa, wilaya na Kamati za Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kujionea namna mfumo huo unavyotekelezwa kwenye zao la ufuta.

“Nimeridhishwa na namna serikali za mikoa zinavyoendelea kushirikiana na WRRB katika kuhakikisha mfumo unasimamiwa vizuri. Viongozi wote tuliokutana nao wameonesha utayari mkubwa wa kusimamia utekelezaji wa mfumo huu na kushughulikia changamoto zinazojitokeza,” amesema.

Amesema moja ya maelekezo makubwa yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika mfumo huo hazitumiki kama sababu ya kurejea katika biashara holela ya mazao, bali zitafutiwe ufumbuzi kwa wakati.

Kwa mujibu wa Bw. Bangu, changamoto zilizotajwa na Waziri Mkuu zinahusisha miundombinu ikiwamo ujenzi wa maghala, matengenezo ya barabara na uwepo wa mazingira bora ya kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayopitia katika mfumo huo. Amesema WRRB imeweka mikakati mahsusi ya kuhakikisha ubora wa mazao unaimarishwa kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na wilaya ili bidhaa zote zinazopelekwa maghalani zikidhi viwango vinavyotakiwa.

“Tumewaelekeza waendesha maghala kuzingatia kikamilifu miongozo iliyotolewa na taasisi husika. Kwa sasa zao lililo sokoni ni ufuta na tayari miongozo ya utekelezaji imetolewa na COPRA,” amesema.

Kuhusu upungufu wa maghala, Bw. Bangu amesema tayari WRRB imeanza mazungumzo na halmashauri mbalimbali ili kuona namna ya kutumia fursa ya uwekezaji katika miundombinu ya maghala ambayo itaongeza ufanisi wa mfumo huo na kuwafikisha wakulima karibu zaidi na minada.

Kadhalika, amesema WRRB kwa kushirikiana na COPRA pia imeanza kuangalia uwezekano wa kuongeza mazao mengine kwenye mfumo ikiwamo karanga, njugu mawe na choroko ili kuongeza idadi ya wanufaika.

Akizungumzia changamoto ya mdororo wa bei, Bangu amesema wananchi wamekuwa wakilinganisha bei za sasa na zile za miaka mitatu iliyopita bila kuzingatia mabadiliko ya soko la dunia, hivyo WRRB imeendelea kutoa elimu kuhusu mwenendo wa bei katika masoko ya kimataifa.

Pia amesema baadhi ya maeneo yamekumbwa na upungufu wa uzalishaji kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na ukosefu wa mbegu bora, na kwamba WRRB imeanza mazungumzo na Jeshi la Magereza ili kutumia mashamba yake kuongeza uzalishaji wa mbegu.

“Niwahakikishie wananchi kuwa mfumo huu ni imara na tunaendelea kutatua changamoto zote zinazojitokeza. Tukishirikiana na wadau wote, tutamkomboa mkulima wa Tanzania na kuhakikisha anapata thamani halisi ya mazao yake,” alisema.

0/Post a Comment/Comments