TANZANIA YAJIPANGA KUNUFAIKA NA MAPINDUZI YA AKILI UNDE

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Pili kuhusu Maendeleo ya Akili Bandia katika Muktadha wa Afrika (AAIAC 2026), uliofanyika Julai 21, 2026 jijini Dar es Salaam.

                                                  *******

SERIKALI imesema  kuwa Tanzania  inaendelea kuwekeza katika maandalizi ya wataalamu wa Akili Bandia (AI) ili kutumia teknolojia hiyo kuongeza maendeleo ya taifa na kushindana katika mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea duniani.

Hatua hiyo imeelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Pili kuhusu Maendeleo ya Akili Bandia katika Muktadha wa Afrika (AAIAC 2026), uliofanyika Julai 21, 2026 jijini Dar es Salaam.

Profesa Mkenda amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali, Ajenda ya Utafiti wa Taifa na Mpango wa Ufadhili wa Samia kwa lengo la kuandaa wataalamu wenye uwezo katika sayansi ya data, akili bandia na teknolojia nyingine za kisasa.

Amesema kupitia programu hizo, Tanzania imeanza kuwekeza katika kuwaandaa wataalamu wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali duniani ili kurejesha ujuzi huo na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Uwekezaji huu katika programu za sayansi ya data na akili bandia utaimarisha uwezo wa taifa na kuchangia nafasi ya Afrika katika mapinduzi ya kidijitali,” amesema Profesa Mkenda.

Waziri huyo amesema pamoja na fursa kubwa zinazotokana na AI katika sekta kama afya, elimu, kilimo na biashara, matumizi ya teknolojia hiyo yanapaswa kuzingatia usalama wa taarifa binafsi na maadili ili kuepusha madhara kwa jamii.

Akizungumzia sekta ya elimu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Gloriana Monko, amesema AI imekuwa msaada kwa wanafunzi kwa kurahisisha upatikanaji wa vitabu na nyenzo mbalimbali za kujifunzia.

Hata hivyo, amesema wanafunzi hawapaswi kutegemea AI kama chanzo pekee cha majibu, bali waitumie kama nyenzo ya kuongeza uelewa, kufanya uchambuzi na kukuza uwezo wa kufikiri.

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Gloriana Monko  Akizungumza wakati wa ufunguaji wa  Mkutano wa Kimataifa wa Pili kuhusu Maendeleo ya Akili Bandia katika Muktadha wa Afrika (AAIAC 2026), uliofanyika Julai 21, 2026 jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lughano Kusiluka, amesema vyuo vikuu vina wajibu wa kuwaandaa vijana kutumia AI kwa usahihi ili waweze kushiriki katika maendeleo ya teknolojia hiyo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Lughano Kusiluka Akizungumza wakati wa ufunguaji wa  Mkutano wa Kimataifa wa Pili kuhusu Maendeleo ya Akili Bandia katika Muktadha wa Afrika (AAIAC 2026), uliofanyika Julai 21, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema AI tayari inaanza kubadili sekta mbalimbali na Tanzania inapaswa kuendelea kuwekeza katika teknolojia mpya ikiwemo kompyuta za quantum ili kujenga kizazi cha wataalamu kitakachoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.








Picha ya pamaja  wakati wa ufunguaji wa  Mkutano wa Kimataifa wa Pili kuhusu Maendeleo ya Akili Bandia katika Muktadha wa Afrika (AAIAC 2026), uliofanyika Julai 21, 2026 jijini Dar es Salaam.

0/Post a Comment/Comments