TANZANIA YAUNGA MKONO MPANGO WA KUKOMESHA MATUMIZI YA ZEBAKI IFIKAPO 2032

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma Takribani watoto 10,000 nchini wanahusishwa na shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu zinazotumia zebaki  hali inayowaweka katika hatari  ya kupata madhara ya kiafya kutokana na sumu ya kemikali hiyo. Mbali na watoto, wanawake  kati ya asilimia 20 hadi 30  katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini pia wanakabiliwa na athari kubwa za kiafya zinazotokana na matumizi ya zebaki, ikiwemo madhara ya mfumo wa fahamu na afya ya uzazi. Hali hiyo imechochea wadau wa mazingira kutaka biashara ya zebaki duniani ikomeshwe na matumizi yake katika uchimbaji mdogo kusitishwa ifikapo mwaka 2032. Akizungumza leo Julai 30, 2026 jijini Dodoma katika Warsha ya Mradi wa Marekebisho ya Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki unaotekelezwa na AGENDA kwa kushirikiana na IPEN,Afisa Programu wa AGENDA, Angel Shaniva amesema mbali na kuhusisha watoto, sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu (ASGM) inakadiriwa kuajiri moja kwa moja zaidi ya watu milioni 1.2 huku zaidi ya watu milioni 7.2 wakitegemea shughuli zake kwa njia zisizo za moja kwa moja. Shaniva amesema jamii inapaswa kuachana na matumizi ya zebaki (mercury) ili kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya athari za kiafya na kimazingira.  Amesema mradi huo unalenga kuongeza uelewa na kujenga ushirikiano kati ya wadau wote ili kuharakisha utekelezaji wa Mkataba wa Minamata na kuunga mkono marekebisho yanayolenga kukomesha biashara ya zebaki duniani pamoja na kuweka tarehe rasmi ya kusitisha matumizi yake katika uchimbaji mdogo wa dhahabu. Amesema AGENDA imekuwa ikifanya kazi katika maeneo ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi, elimu na jinsia, ambapo kupitia zaidi ya miradi 140 iliyotekelezwa imeendelea kukuza ushirikiano na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya maendeleo endelevu. Kwa upande wake Afisa Program wa AGENDA, Clara Benjamin, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 153 wanachama wa Mkataba wa Minamata unaolenga kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara ya zebaki, lakini bado biashara ya kemikali hiyo inaendelea huku kukiwa hakuna tarehe rasmi ya kusitisha matumizi yake katika uchimbaji mdogo wa dhahabu. Amesema takwimu zinaonyesha biashara ya zebaki duniani imeongezeka kutoka tani 1,200 mwaka 2017 hadi tani 1,700 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 40, huku sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu ikiendelea kutumia zaidi ya tani 2,000 za zebaki kila mwaka bila dalili za kupungua. Kwa mujibu wake, maeneo yenye matumizi makubwa ya zebaki nchini ni Geita, Shinyanga, Mbeya na Mara ambako kemikali hiyo hutumika kutenganisha dhahabu, lakini matumizi hayo yameendelea kusababisha uchafuzi wa ardhi, mito na samaki pamoja na madhara makubwa ya kiafya ikiwemo uharibifu wa mfumo wa fahamu na kuhatarisha usalama wa chakula. Amesema matumizi ya zebaki pia yanahusishwa na biashara haramu ya dhahabu, kuikosesha Serikali mapato na kudhoofisha usimamizi wa sekta ya madini. Amesema marekebisho yanayopendekezwa katika Mkataba wa Minamata yanataka biashara ya kimataifa ya zebaki ipigwe marufuku isipokuwa kwa matumizi yanayokubalika kimazingira pamoja na kuweka mwaka 2032 kuwa mwisho wa matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu. Kwa upande wake, Afisa Mazingira Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Ahmad Hassan Mbwana, amesema Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine imeendelea kutekeleza miradi ya kupunguza matumizi yasiyo salama ya zebaki kupitia utoaji wa elimu katika mikoa saba ikiwemo Mwanza na Geita. Amesema wachimbaji wadogo wameendelea kuelimishwa kuhusu madhara ya zebaki, matumizi ya teknolojia salama na umuhimu wa kufanya tathmini za athari kwa mazingira kabla na wakati wa shughuli za uchimbaji. Mbwana amesema elimu hiyo imechangia kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na pia kuongeza tija ya uzalishaji kwa wachimbaji wanaotumia teknolojia salama, huku uratibu wa wadau na mapitio ya sheria mbalimbali ukiendelea kuboreshwa. Hata hivyo amesema bado ipo changamoto ya baadhi ya wachimbaji kutokuwa na anuani rasmi za maeneo yao ya kazi, hali inayofanya kuwa vigumu kuwafikia kwa ajili ya ukaguzi wa usalama, utoaji wa elimu na ufuatiliaji wa matumizi ya kemikali hatarishi. Naye Mkaguzi wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Thadei Mwasamila, amesema ni muhimu kuimarisha ukaguzi wa mara kwa mara katika migodi midogo, kubaini vihatarishi na kuhakikisha wachimbaji pamoja na waajiri wanazingatia viwango vya afya na usalama kazini. Amesema OSHA itaendelea kusisitiza matumizi sahihi ya vifaa vya kinga binafsi, uhifadhi salama wa kemikali na usimamizi wa taka zenye zebaki ili kupunguza madhara ya muda mrefu kwa wachimbaji na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NESODO, Alfred Lugela, amesema kupanda kwa bei ya dhahabu duniani kumeongeza matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo, huku akieleza kuwa udhibiti wa biashara ya kemikali hiyo unaweza kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala zilizo salama. Kutokana na hayo Mhandisi wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Yusuf Yusufu, amesema usimamizi madhubuti wa shughuli za uchimbaji mdogo pamoja na matumizi ya teknolojia mbadala kama gravity concentration na borax ni muhimu katika kulinda afya za wananchi, mazingira na kuongeza tija katika sekta ya madini. Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Tawfiq Halfan, amesema mafanikio ya kupunguza matumizi ya zebaki yatategemea ushirikiano wa Serikali, wadau wa mazingira, wachimbaji na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika bila kuhatarisha afya za wananchi na mazingira. Kwa mujibu wa wadau hao, kuungwa mkono kwa marekebisho ya Mkataba wa Minamata kutaiwezesha Tanzania kupunguza matumizi ya zebaki, kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kulinda afya za wachimbaji, wanawake, watoto na vizazi vijavyo.

            

0/Post a Comment/Comments