WAZAZI WATAKIWA KUANZA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NYUMBANI

********

MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amewataka wazazi kuwapa watoto elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya tangu wakiwa wadogo ili kuwajengea uwezo wa kukataa vishawishi.

Amesema vijana wengi huanza kutumia dawa za kulevya wakiamini ni fasheni au starehe, lakini baadaye huingia kwenye uraibu unaoharibu maisha yao na mustakabali wa taifa.

Mapunda amesema njia bora ya kukomesha biashara ya dawa za kulevya ni kukata mnyororo wa biashara hiyo kwa kupunguza idadi ya watumiaji, kwa kuwa uhitaji ndiyo unaochochea usambazaji.

Amesema hayo leo Julai 23, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la kuhamasisha jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Amesema alipoitembelea banda la DCEA alioneshwa sampuli za dawa za kulevya zilizotengenezwa kwa muonekano wa keki na kwamba baadhi yake hutumiwa na wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu katika sherehe binafsi.

Pia amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuimarisha ufuatiliaji wa mitandao ya biashara ya dawa za kulevya na mifumo ya utakatishaji fedha, huku akionya kuhusu maisha ya anasa yanayooneshwa mitandaoni.

Aidha, amesema tabia ya kuonesha fedha nyingi bila kueleza zilivyopatikana inaweza kuwavutia vijana kutafuta utajiri wa haraka na kujiingiza kwenye biashara haramu.

Mapunda amesema vita dhidi ya dawa za kulevya vitafanikiwa ikiwa wananchi watatoa taarifa kwa mamlaka na serikali, wazazi, vijana pamoja na jamii kwa ujumla watashirikiana kulinda kizazi cha sasa na kijacho.

















0/Post a Comment/Comments