Na Daniel Limbe, Karagwe
"Maisha ni Hesabu" hiyo ni nukuu ya mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kayanga, Almachius Rweyongeza.
Alikuwa akiwahusia wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2026 kwenye shule ya wasichana ya Mavuno iliyopo kijiji cha Chonyonyo wilayani Karagwe mkoani Kagera.
Mbali na nukuu hiyo, amewataka wahitimu wote nchini kuziishi KKK akimaanisha Kusoma, Kuhesabu na Kuandika huku akiwasisitiza kujenga mazoea ya kusoma magazeti na vitabu vitakatifu vya Biblia na Quran ili kuendelea kujaza mbolea ya maarifa katika nafsi zao.
Askofu Rweyongeza, ametumia maneno ya Kitabu kitakatifu cha Biblia kuonyesha kuwa kumcha Bwana ndiyo chanzo kikuu cha kuwa na maarifa ya kibinadamu na kwamba maisha pasipo kuacha alama ni sawa na bustani iliyotelekezwa na kuzongwa na magugu.
Hata hivyo amemwaga sifa kedekede kwa Mkurugenzi wa shirika lisilo la Kiserikali la Mavuno, kwa kutambua thamani ya elimu na kulazimika kuanzisha shule ya wasichana ambao awali walikuwa hawapewi kipaumbele cha kupata elimu katika jamii.
Pia amepongeza maono ya taasisi hiyo kwa kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, huku akiitaka jamii kutambua thamani ya kuacha alama (kumbukumbu) zisizofutika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
"Elimu pasipo kujiendeleza ni sawa na bustani iliyosongwa na magugu" hivyo wahitimu wote nchini wanapaswa kuendelea kujisomea ili jamii inufaike na ujuzi na maarifa yao badala ya kuonekana wajinga.
Mbali na mambo mengine, Askofu Rweyongeza amebariki majengo mapya ya ghorofa kwaajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita na kuwataka wazazi na walezi kujivunia uwepo wa shule hiyo katika maeneo yao.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Charles Bahati, amesema wanajivunia kuwa na shule bora kwenye wilaya ya Karagwe na mkoa wa Kagera kutokana na umahili na ustadi mkubwa wa kitaaluma unaopatikana kwenye shule hiyo.
Amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea shirika hilo ili liweze kufikia ndoto za kutoa elimu bora zaidi hali itakayosaidia vijana kupambana vyema katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Ameshukuru kwa ushirikiano uliopo kati ya jamii, serikali na washirika wenza wakiwemo marafiki wa afrika kutoka nchini Sweden pamoja na Ujerumani ambao wamekuwa wakiendelea kulisaidia shirika hilo kwa muda mrefu.
Kw upande wake mkuu wa shule hiyo, Gloria Herman, ametumia fursa hiyo kuwasihi wahitimu kuishi maisha yenye maadili wakati wote badala ya kuingia mitaani na kuiga tabia mbaya ambazo zitasababisha kutwezwa utu wao.
Aidha amesema shule hiyo ina wanafunzi 106 ambao wanatarajia kuhitimu kidato cha nne mwaka 2026, huku akijiandaa na usajili wa wanafunzi wa kidato cha tano na sita mwaka huu.
Ipo nukuu ya aliyekuwa Rais wa Afrika ya kusini Nelson Mandela ikisema " Elimu ni silaha yenye nguvu yenye kuweza kuibadili dunia".





Post a Comment