........
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkoa wa Dodoma umejipanga kuwafikia zaidi ya watoto milioni moja wenye umri chini ya miaka 10 kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya Matone ya Polio, inayolenga kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa huo na kuzuia uwezekano wa maambukizi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Agosti 26, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema jumla ya watoto 1,003,461 wanatarajiwa kupata chanjo hiyo katika awamu mbili za kampeni.
Amesema awamu ya kwanza itafanyika kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2026, huku awamu ya pili ikitarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2, 2026, ambapo watoto walewale watafikiwa katika awamu zote mbili.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, chanjo itatolewa katika maeneo mbalimbali ambako watoto wanapatikana, yakiwemo shule, vituo vya afya, nyumba za ibada na kupitia mfumo wa nyumba kwa nyumba.
Mkoa wa Dodoma umeandaa jumla ya timu 2,001 za uchanjaji, kila moja ikiwa na mchanjaji, mtunza takwimu pamoja na mhamasishaji, ili kuhakikisha kampeni hiyo inawafikia watoto wote wanaostahili.
Mhe. Senyamule amesema kampeni hiyo haimaanishi kuwa kuna mlipuko wa Polio katika Mkoa wa Dodoma, bali ni hatua ya tahadhari inayolenga kuimarisha kinga ya watoto kufuatia kubainika kwa hatari ya virusi vya Polio kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huo.
Amesema Tanzania imepita takribani miaka 30 tangu Julai 1996 bila kuripotiwa mgonjwa wa mwisho aliyethibitika kuwa na virusi vya Polio, lakini hali hiyo haiwezi kuwa sababu ya kusitisha juhudi za kinga na ufuatiliaji.
“Hadi sasa hakuna mtoto aliyethibitika kuugua ugonjwa wa Polio ndani ya Mkoa wa Dodoma. Kampeni hii ni hatua ya tahadhari ya mapema inayolenga kuimarisha kinga ya watoto na kuzuia uwezekano wa maambukizi,” amesema.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote walio chini ya miaka 10 wanapatiwa chanjo hiyo bila kujali kama wamekamilisha ratiba yao ya kawaida ya chanjo.
Amesisitiza kuwa chanjo ya Polio ya matone ni salama na inatolewa bila malipo, huku akiwataka wananchi kuendelea kuzingatia usafi wa mazingira na binafsi, ikiwemo matumizi sahihi ya vyoo na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “MPE CHANJO MTOTO WAKO. LINDA TABASAMU LA MTOTO. ZUIA POLIO.”
Mkoa wa Dodoma umeweka malengo maalumu kwa kila halmashauri, ambapo Dodoma Jiji inaongoza kwa lengo la kuwafikia watoto 207,096, ikifuatiwa na Chamwino 169,408, Kongwa 151,386, Mpwapwa 135,907, Chemba 119,631, Bahi 115,909, Kondoa 80,465 na Kondoa Mji 23,659.
Mhe. Senyamule pia ametoa wito kwa viongozi wa dini, viongozi wa jamii, walimu, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na vyombo vya habari kushirikiana na Serikali kuhakikisha ujumbe wa kampeni unawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema kinga ni bora kuliko tiba, hivyo wananchi hawapaswi kusubiri ugonjwa kujitokeza ndipo waanze kuchukua hatua za kuwalinda watoto wao.






Post a Comment