WANAWAKE WA KIISLAMU WAHIMIZA USHIRIKIANO KUWALINDA WATOTO KIAFYA


Mwenyekiti wa taasisi  ya Muslima Medical Support Fund (MMSF), Dk. Asha Mahita Akizungumza na vyombo vya habari kando ya mkutano mkuu wa mwaka.
********
Umoja wa madaktari wanawake Waislamu nchini kupitia Taasisi ya Muslima Medical Support Fund (MMSF) umeendelea kuimarisha jitihada za kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zenye uhitaji.

Akizungumza na vyombo vya habari Jana Augusti 1,2026 jijini Dar es Salaam, katika mkutano mkuu wa mwaka Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Dk.Asha Mahita amesema lengo la kufanya hayo kwa watoto ni kuhakikisha wanaisaidia Serikali kuhakikisha kila mtanzania ana haki ya kupata matibabu kwa kuwa afya ya mtoto wa leo ndio nguvu ya Taifa ya kesho.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dk. Asha Mahita, amesema tangu kuanzishwa mwaka 2020, watoto zaidi ya 850 wamepatiwa bima ya afya.

Amesema hatua hiyo imewawezesha watoto wengi kupata huduma za matibabu kwa wakati bila familia zao kubeba gharama kubwa.

Mbali na bima, amesema taasisi imechangia matibabu ya watoto zaidi ya 150 waliokuwa na changamoto ambazo hazikugharamiwa na bima.

Dk. Mahita amesema zaidi ya Sh95 milioni zimekusanywa na kuelekezwa katika kugharimia bima na huduma za matibabu kwa watoto nchini.

Amesema taasisi pia imejikita kutoa elimu kuhusu afya ya akili na ukomo wa hedhi pamoja na kuhamasisha jamii kuchangia bima za afya.

Aidha, amesema bado kuna watoto wengi wanaohitaji msaada, huku zaidi ya maombi 20 yakisubiri kupatiwa bima.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha watoto wengi zaidi wanafikiwa na huduma hizo.

Kwa upande wake, mgeni rasmi Mwantumu Malale amepongeza juhudi za taasisi hiyo akisema zinaunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Katika mkutano mkuu wa mwaka wa MMSF, wanachama na wadau walichangisha zaidi ya Sh3 milioni, Euro 100 na Dola za Marekani 200 kwa ajili ya kuwakatia bima watoto wengine wenye uhitaji.












0/Post a Comment/Comments