WAZIRI WA FEDHA AZITAKA TAASISI ZA FEDHA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA KILIMO

*******
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ametembelea Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane leo jijini Dodoma na kubainisha kuwa, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni lazima kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo.

Waziri Balozi Khamis amebainisha hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akitembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa na Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni.

Amesema kuwa, kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutategemea kwa kiwango kikubwa mafanikio ya sekta ya kilimo. Hivyo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inapaswa kuelekeza uwekezaji wake katika maeneo ya kimkakati yatakayoongeza tija na kukuza sekta hiyo.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mtaji wa TADB kutoka Sh bilioni 60 hadi zaidi ya Sh bilioni 400, ili benki hiyo iweze kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu, ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa taifa.

Waziri Omar amesema Serikali inalenga kutumia maendeleo ya sekta hizo kupunguza umaskini, kuongeza kipato cha wananchi na kufikia lengo la uchumi wa dola trilioni moja kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, aliwataka viongozi wa Wizara ya Kilimo kuendelea kuwatafutia masoko wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini, huku wakiongeza juhudi za kuwawezesha kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.

Pia aliipongeza Wizara hiyo kwa kazi inayoendelea kufanya katika kuendeleza sekta ya kilimo na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta za mifugo na uvuvi ili kuongeza tija, ajira, usalama wa chakula na kipato cha wananchi.



0/Post a Comment/Comments