********
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ameipongeza TTCL kwa hatua inazochukua katika kuboresha na kuendeleza huduma za mawasiliano ya kidijitali nchini.
Kairuki ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Kituo Jumuishi cha TTCL cha Faiba (FTTX Experience Centre) kilichopo Kijitonyama, ambapo amejionea huduma na suluhisho mbalimbali za mawasiliano zinazotolewa kupitia teknolojia ya FTTH/FTTX.
Amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali yamekuwa muhimu katika biashara, elimu, huduma za kijamii na utoaji wa huduma za Serikali, hivyo Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa miaka 10 wa mageuzi ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, mpango huo unalenga kuhakikisha wananchi wanaelewa na kutumia teknolojia, sambamba na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kidijitali.
Amesema Tanzania imefikia asilimia 47 ya matumizi ya simu janja, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma za kidijitali zinazoanzishwa zinaendana na uwezo wa wananchi kuzitumia.
Aidha, Kairuki amesema TTCL imepiga hatua katika huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), huku ikiendelea kupanua huduma hiyo katika nyumba za kisasa kupitia teknolojia ya Smart Home.
“Tunawakaribisha sana Watanzania wote, kwa rika zote. TTCL imejipanga vizuri sana na tumeshafanya mambo makubwa. Sasa hivi siyo TTCL ambayo mmeijua ya wakati ule, imebadilika sana katika utoaji wa huduma zake,” amesema Kairuki.
Amesema changamoto katika utoaji wa huduma haziwezi kukosekana kutokana na ongezeko la watumiaji, lakini TTCL imeendelea kuboresha mifumo yake, ikiwamo huduma kwa wateja.
Ameongeza kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaendelea kuwa muhimu katika kuongeza kasi ya intaneti na kupunguza gharama za huduma za mawasiliano nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema shirika hilo limepanga kuongeza maungio ya Faiba Mlangoni Kwako hadi takribani 750,000 ifikapo Juni 2027, kutoka maungio 330,000 yaliyopo sasa.
Marwa amesema wateja wapatao 115,000 tayari wamejiunga na huduma hiyo, huku TTCL ikiendelea na mikakati ya kuifikisha huduma ya intaneti ya kasi kwa Watanzania wengi zaidi.
















Post a Comment