KONGOLE RUWASA KWA ITHIBATI, PAMBANENI KUFIKISHA MAJI KATIKA VIJIJI 1,575

.........

NA: DK. REUBENI LUMBAGALA 

Maji ni huduma muhimu katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu anahitaji maji kwa matumizi kadha wa kadha kijamii na kiuchumi. Kutokana na umuhimu wa maji, serikali haijalala. 

Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha fedha zinapatikana za kugharamia miradi ya maji, huku usimamizi madhubuti ukiimarishwa kwa miradi inayoendelea kutekelezwa ili ikamilike na hatimaye itoe huduma kwa wananchi.

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ni taasisi muhimu katika Wizara ya Maji. Ni wadau muhimu wanaoratibu usambazaji maji vijijini ili kuhakikisha wananchi waishio maeneo hayo wanapata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Pamoja na mambo mengine, RUWASA imepata mafanikio makubwa kutokana na utoaji na usambazaji wa huduma bora za maji vijijini kwa viwango vya juu vya ubora kimataifa. Hii imesababisha RUWASA kupata ithibati ya kimataifa ya: ISO 9001:2015.

Ithibati hiyo ni kielelezo cha huduma bora zinazotolewa na RUWASA katika kuwahudumia wananchi hasa waishio vijijini. Mathalani, kumekuwa na kasi kubwa ya usambazaji maji vijijini na ndiyo maana upatikanaji wa maji vijijini kwa sasa umefikia asilimia 85.2. 

Hivi karibuni, Jijini Dodoma, katika Kikaokazi na Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti pamoja na Mameneja wa RUWASA wa mikoa na wilaya, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliwahimiza RUWASA, kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata maji.

Aweso alisisitiza kuwa, katika vijiji 12,333 vilivyopo nchini, ni vijiji 1,575 tu ndiyo bado havijafikiwa kikamilifu na huduma ya maji, hivyo, RUWASA kama wakala mwenye dhamana ya usambazaji wa maji vijijini, wanao wajibu kuhakikisha vijini 1,575 vilivyobaki zinapata maji ya uhakika ifikapo mwaka 2030.

Kimsingi, pamoja na maji kuwa huduma ya kijamii, lakini maji ni uchumi na yana mnyororo mkubwa katika kuchechemua maendeleo ya uchumi, na hivyo kuchangia kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Mafanikio ya sekta ya maji, yanachangia kukua kwa sekta za kilimo, uvuvi, uzalishaji wa nishati ya umeme na huduma bora za kijamii kama elimu na afya.

Sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuwezesha kasi ya usambazaji wa maji vijijini, hivyo ishiriki kikamilifu katika kuiunga mkono serikali kwani ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP), ndiyo mwelekeo wa serikali katika kuharakisha maendeleo ikiwemo sekta ya maji.






 

0/Post a Comment/Comments