MATAIFA 48 KUTUA ARUSHA KWA MKUTANO WA CATA, WAGENI ZAIDI YA 100 KUTALII TANZANIA - RC ARUSHA

*******

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA. Amos Makalla amesema zaidi ya wajumbe 100 kutoka mataifa 48 wanatarajiwa kuwasili jijini Arusha kuhudhuria Mkutano wa 46 wa Wakuu wa Mamlaka za Kodi za Jumuiya ya Madola (CATA), unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.

Ameyasema hayo leo Septemba 30, 2026 jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano wa 46 wa CATA utakaofunguliwa Rasmi na Mgeni Rasmi ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, Oktoba 6 jijini Arusha katika Hoteli ya Grand Melia.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo inalenga matumizi ya teknolojia katika kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, hivyo Tanzania itapata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali zinazotumiwa na mamlaka za kodi za nchi nyingine.

Aidha, ameongeza kuwa ushiriki wa wataalamu kutoka mataifa mbalimbali utasaidia kujenga uwezo wa wataalamu wa TRA na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, hasa kutokana na kuongezeka kwa biashara zinazovuka mipaka.

Mbali na hayo, CPA Makalla amewataka wananchi na watoa huduma Arusha kutumia fursa hiyo kuwahudumia wageni kwa ukarimu na upendo, akisema wajumbe hao watatumia hoteli, usafiri na huduma mbalimbali wakati wa kukaa jijini humo.

CPA Makalla ameitumia nafasi hiyo kuipongeza TRA kwa kuaminiwa kuwa mwandaaji na mwenyeji wa mkutano huo, huku akitangazaMakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ndiye atakayekuwa mgeni rasmi na anatarajiwa kuufungua mkutano huo Oktoba 6 jijini Arusha.

Kwa upande wake Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Mcha Hassan Mcha akizungumza kuhusu yale yatakayojadiliwa katika mkutano huo wa 46 wa CATA, amefafanua kuwa huduma kwa walipakodi ni miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa, kwa kuwa viwango vya huduma hutofautiana kati ya nchi na nchi, huku TRA ikilenga kujifunza ili kufikia viwango vya kimataifa katika kuwahudumia walipakodi nchini.

Sambamba na hayo, amesema mkutano huo utajadili uchumi wa kidijitali na biashara zinazofanyika kupitia mitandao, pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu utakaosaidia mamlaka za kodi kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia.












 

0/Post a Comment/Comments