Na Mwandishi Wetu, Ruvuma.
Wahitimu wa mafunzo ya Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) wametakiwa kutumia ujuzi walioupata kwa maslahi mapana ya Taifa pamoja na kuwaelimisha wananchi namna ya kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
Wito huo umetolewa na Afisa Wanyamapori Mkuu Mkoa wa Ruvuma, Bw. Ernest Nombo, alipokuwa akifunga mafunzo ya wahitimu hao katika Chuo cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga, Mkoani Ruvuma.
Bw. Mombo amesema migongano hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, kutosimamiwa vizuri kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kuzibwa kwa mapito ya wanyamapori, hali inayowafanya wanyamapori kuingia katika mashamba na makazi ya wananchi.
Amesema wahitimu hao wamefundishwa kuwa walimu na walinzi wa rasilimali za taifa katika jamii wanazotoka na si vinginevyo.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho, mwaka 1965, zaidi ya watu 5,000 wamepata mafunzo mbalimbali yanayohusu uhifadhi, hatua ambayo imekuwa na mchango katika kuimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali za maliasili katika vijiji wanakotoka.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, World Wide Fund For Nature (WWF) na wadau wengine kwa kuendelea kuwezesha mafunzo hayo.
Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga, Joshua Dotto Simion, amesema Askari Wanyamapori Wasaidizi 42 wamehitimu Kozi Na. 79 ya mwaka 2026, baada ya kupata mafunzo kwa kipindi cha miezi mitatu tangu Juni 15, mwaka huu.
Amesema washiriki hao wametoka Nachingwea, Liwale, Rufiji na Sumbawanga, huku 40 wakifadhiliwa na WWF na wawili na Wizara.
Bw. Simion amefafanua kuwa wahitimu hao wamejengewa uwezo katika mbinu za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, usimamizi wa maliasili, matumizi ya GPS na ramani, huduma ya kwanza, sheria za uhifadhi, ufugaji nyuki, mbinu za kuishi porini na haki za binadamu, ili waweze kutoa mwitikio wa haraka katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za wanyamapori.
Naye Mhitimu Majidi Hashimu Manyigu, kutoka Ngarambe Mashariki, Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, amesema mafunzo hayo yamempa uwezo wa kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu udhibiti wa tembo, nyati na nguruwe kwa kutumia mbinu rafiki kama mizinga ya nyuki na tofali la pilipili.
Ameongeza kuwa atakuwa balozi wa mafunzo hayo katika jamii yake na ameiomba Serikali kuongeza ufadhili ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya mafunzo hayo.






Post a Comment