MALARIA YATISHIA MAENDELEO YA WATOTO AFRIKA


******

Wataalamu wa afya wameonya kuwa maambukizi ya malaria yanayojirudia kwa watoto yanaathiri ukuaji wao, elimu na ustawi wa familia, huku wakitaka juhudi zaidi za kukabiliana na ugonjwa huo barani Afrika.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2025, watoto walio chini ya miaka mitano ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya malaria barani Afrika.

Mwanasayansi Kiongozi wa Mradi wa Transmission Zero katika Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Brian Tarimo, amesema malaria haiathiri afya pekee, bali pia maendeleo ya watoto na uwezo wao wa kujifunza.

Amesema watoto wanaweza kuugua malaria mara kadhaa kwa mwaka, hali inayoongeza changamoto kwa wazazi, walezi, shule na jamii kwa ujumla.

Dk Tarimo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya tafiti za mbinu mpya za kuzuia malaria, akieleza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kulinda afya na mustakabali wa kizazi kijacho.

Nchini Tanzania, IHI na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kwa kushirikiana na Imperial College London na Swiss Tropical and Public Health Institute, zinaendeleza utafiti wa teknolojia ya gene drive kupitia Mradi wa Transmission Zero.

Teknolojia hiyo inalenga kutumia mabadiliko ya kijenetiki kwa mbu ili kuzuia usambazaji wa vimelea vya malaria. Kwa sasa, tafiti hizo zinafanyika katika mazingira ya maabara yenye udhibiti madhubuti nchini Tanzania.

Taarifa ya Transmission Zero imeeleza kuwa Afrika inachangia takribani asilimia 94 ya visa vya malaria duniani, hivyo kuimarisha juhudi za kuzuia ugonjwa huo ni muhimu katika kulinda afya za watoto na maendeleo ya jamii.









0/Post a Comment/Comments