Mgombea ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia Chama cha United Democratic Party (UDP), Hasma Judi Hamisi, amewaomba wananchi kumchagua kwa kuwa ni kijana mwenye nguvu za kuwatumikia, akiahidi kushughulikia elimu, afya, maji na mikopo kwa makundi ya wajasiriamali wadogo.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika Chamwino, Hasma alisema ameteuliwa na UDP kupeperusha bendera ya chama hicho, na kwa idhini ya wananchi anaamini atawatumikia vyema.
"Nimejipanga kuwatumikia vizuri, kwa weledi, kwa ufasaha na kwa wakati sahihi," alisema.
Akifafanua vipaumbele vyake, Hasma alisema jambo la kwanza ni elimu, akiahidi kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya kwenda shule. Alisema atasitisha michango ya shule isiyo ya lazima kwa kushirikiana na walimu.
Kwa upande wa afya, alisema atahakikisha kila kijiji ndani ya jimbo hilo kinakuwa na zahanati, hasa kwa ajili ya huduma za afya ya mama na mtoto.
Kuhusu maji, alisema amefanya utafiti na kubaini changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo hilo, hivyo atahakikisha wananchi wa Chamwino wanapata maji safi na salama.
Hasma alisema hatawasahau wafanyabiashara wadogo (machinga), mama ntilie na waendesha bodaboda, akiahidi kusimamia upatikanaji wa mikopo isiyo na riba kubwa wala usumbufu, pamoja na kuwawekea mikakati bora ya kiuchumi.
"Ninachohitaji ni kura zenu, mnichague kijana mwenzenu katika kuleta maendeleo," alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UDP Taifa, Saumu Rashid, alisema licha ya tofauti za kisiasa kati ya vyama, wote wapo pamoja kwa masilahi ya taifa la Tanzania, huku akisisitiza amani na utulivu.
Akiwasilisha salamu "Pigeni kura kwa usahihi, kisha rudini nyumbani mkisubiri matokeo. Tunaamini mshindi atakayepatikana ndiye mshindi wa wana Chamwino," alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema ilani ya UDP inalenga kukuza uchumi wa wananchi wa kawaida, akibainisha kuwa wakazi wa Chamwino, Dodoma, ni wakulima wa zabibu, na chama hicho kimeainisha mikakati ya kuwainua wakulima hao.
Alisema Hasma akiingia bungeni atakuwa na jukumu kubwa la kusimamia mambo yanayoinua uchumi wa wananchi wa Chamwino. Kwa kuwa zabibu ni zao la kimkakati, alisema lengo ni kuboresha miundombinu ya soko la uhakika ili zao hilo liwanufaishe wakazi wa jimbo hilo.
Katika uchaguzi huo wa ubunge Chamwino, vyama 16 vimesimamisha wagombea. Vyama ambavyo havina
Na Carlos Claudio, Chamwino.


Post a Comment