MTUMBA YAANZA KUVUTIA WATALII DODOMA SIKU CHACHE KABLA YA UZINDUZI


......

Na Carlos Claudio, Dodoma

Wahariri, wasanii, wanafunzi wa vyuo vikuu na watengeneza maudhui mtandaoni wametembelea Jiji la Serikali Mtumba jijini Dodoma, kabla ya uzinduzi rasmi utakaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 30, 2026.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema uzuri na mpangilio wa jiji hilo vinatoa mafunzo yanayoweza kutumika kuboresha maeneo mengine ya nchi, ikiwemo Dar es Salaam.

Bw Balile aliipongeza serikali, wahandisi na viongozi waliosimamia mradi huo, akiwataja marais walioongoza utekelezaji wake, kuanzia hayati Dkt John Magufuli hadi Dkt Samia Suluhu Hassan.

Wasanii walioshiriki ziara hiyo walisema walivutiwa na ukubwa na ubora wa majengo na miundombinu. Walieleza mradi huo kuwa fursa kwa wasanii, jamii na taifa kwaWaliongeza

Waliongeza kuwa kukamilika kwa jiji hilo kunaonesha hatua iliyopigwa katika kutimiza ndoto ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya shughuli za serikali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema jiji hilo limejengwa kwa kuzingatia mifumo ya kisasa ya utoaji huduma, ikiwemo matumizi ya teknolojia kurahisisha kazi za serikali.

Alisema uwekezaji huo umeifanya Mtumba kuwa jiji la kisasa linaloweza kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi, ambapo wananchi wanaotumia mifumo ya serikali mtandao wanaweza kupata huduma bila kulazimika kwenda kwenye ofisi husika.

Bw Msigwa alisema serikali imejenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 59 ndani ya jiji hilo ili kurahisisha usafiri na kufikika kwa ofisi mbalimbali.

Aliongeza kuwa jiji hilo pia limeanza kuibuka kama kivutio cha utalii mkoani Dodoma, ambapo wageni wanaweza kujifunza kuhusu mpangilio wa majengo yake, miundombinu na mifumo ya kisasa iliyowekwa ili kurahisisha huduma za serikali.

Wakati wa ziara hiyo, washiriki walitembelea ofisi za Wizara ya Madini na kutazama makala fupi kuhusu historia na uanzishwaji wa Jiji la Serikali Mtumba, ambalo linahifadhi taasisi mbalimbali za serikali zinapotekeleza majukumu yake.

Jiji hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan, atakayekuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo.

Ziara hiyo ililenga kuwapa washiriki fursa ya kulifahamu Jiji la Serikali Mtumba na kuelewa historia yake kabla ya uzinduzi rasmi.
 

0/Post a Comment/Comments