TADB YAWEKEZA BILIONI 668 KATIKA KILIMO CHA KAHAWA

*******
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Eliakimu Mnzava, ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa mchango wake katika kukuza kilimo cha kahawa nchini.

Mnzava ametoa pongezi hizo leo, Oktoba 10, 2026, wakati wa kuhitimisha tamasha la Kahawa Festival lililofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha vijana kushiriki katika kilimo cha kahawa, akikitazama kama fursa ya biashara na ajira.

Alipotembelea banda la TADB, alipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa benki hiyo, Alphonce Mokoki, kuhusu uwezeshaji wa kifedha katika mnyororo wa thamani wa kahawa.

Maelezo hayo yalihusu upatikanaji wa mikopo kwa wakulima na wadau wengine wa sekta ya kahawa.

TADB imesema imewezesha jumla ya Shilingi bilioni 668.03 katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 475.83 zimetolewa kupitia mikopo ya moja kwa moja kwa miradi 38.

Mikopo hiyo imewanufaisha watu 313,882, wakiwemo wanawake 61,202 na vijana 54,794.

Aidha, zaidi ya Shilingi bilioni 192 zimewezeshwa kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS), kwa kushirikiana na taasisi washirika za kifedha.

TADB ni benki inayolenga kuwezesha maendeleo ya kilimo nchini kwa kutoa huduma za kifedha kwa wakulima na wadau wa sekta hiyo.



 

0/Post a Comment/Comments