*****
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepanga mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh535.7 bilioni kwa wanafunzi 165,775 katika awamu ya kwanza ya mwaka wa masomo 2026/2027.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alisema katika taarifa iliyotolewa jana kuwa fedha hizo zitawanufaisha wanafunzi wa shahada ya awali, stashahada na wanaoendelea na masomo, pamoja na wanufaika wa Samia Scholarship.
Katika kundi la wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali, wanafunzi 74,769 wamepangiwa mikopo ya Sh246.88 bilioni.
Wanafunzi 8,538 wa stashahada wamepangiwa Sh22.9 bilioni, huku wanafunzi 873 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Sh4.5 bilioni.
Kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo, HESLB imepanga mikopo ya Sh252.4 bilioni kwa wanafunzi 79,115 wa shahada ya awali.
Wanafunzi wengine 1,554 wa stashahada wamepangiwa mikopo ya Sh3.8 bilioni, huku wanufaika 926 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Sh5.1 bilioni.
HESLB imewataka waombaji ambao hawakupangiwa mikopo katika awamu ya kwanza kuendelea kufuatilia maombi yao kupitia mfumo wa _SIPA_ wakati mchakato wa upangaji ukiendelea.
Serikali imetenga Sh1.06 trilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku za wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2026/2027.
Bajeti hiyo inalenga kugharimia wanafunzi 292,463, wakiwamo 111,342 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali.
Pia, wanafunzi 24,978 wa stashahada watanufaika, wakiwamo 14,000 wa mwaka wa kwanza.
Katika mpango wa Samia Scholarship, wanafunzi 2,738 wa shahada ya awali wamejumuishwa, wakiwamo 1,000 wapya.
Aidha, wanafunzi 513 wa Stashahada ya Juu ya Sheria kwa Vitendo wamenufaika katika mpango huo, wakiwamo wanafunzi wapya 350.











Post a Comment