Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameongoza kikao cha pili cha maandalizi ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika AFCON yanayotarajia kufanyika mwaka 2027 na kuwataka wataalamu na wadau wanaoshiriki maandalizi ya mashindano hayo kuandaa mazingira rafiki ikiwemo mifumo ya kidigitali itakayowarahisishia wageni kujua huduma muhimu zinapopatikana
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao hicho Chalamila amesema uwepo wa mifumo ya kidigitali itawarahisishia wageni watakaoingia nchini kwa ajili ya mashindano hayo kujua huduma muhimu zilipo ikiwemo hoteli, vivutio vya utalii na mambo yote muhimu ili kuwawezesha washiriki na wageni wa AFCON kupata huduma muhimu kwa urahisi lakini pia kuimarisha matangazo kuhusu Mkoa huo
Aidha RC Chamamila ametumia kikao hicho kuwataka TARURA na TANROAD kusimamia vyema barabara zimazoendelea kujengwa pamoja na kununua taa za barabarani ili kuboresha mazingira huku pia akizungumzia suala la kuimarisha usafi wa mazingira katika Mkoa huo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya mifumo ya kimataifa ya kuingia viwanjani.
Pia amezungumzia umuhimu wa kuwepo kwa huduma za VVIP kwenye magari ya mwendokasi ili kuwezesha watu wa hadhi mbalimbali kutumia usafiri huo.
Akitoa Taarifa ya Mkoa ya maandalizi ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika AFCON yanayotarajia kufanyika mwaka 2027 Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya AFCON mkoa wa Dar es Salaam Adrophina Ndyeikiza amemhakikishia mkuu wa Mkoa kuwa maandalizi yote ya AFCON yanakwenda vizuri ikiwemo hamasa, kuimarika kwa huduma za afya,uwepo wa App ya ofisi ya Mkoa, uboreshwaji wa viwanja vya mazoezi, huduma za vyakula na kumbi za burudani pamoja na usafi ndani ya Mkoa
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa kikao hicho akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda na Mstahiki Meya wa manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge wameshauri kuimarishwa elimu ya mifumo ya kujaza uwanja kwa njia za kisasa pamoja na kuimarika kwa usafiri wa umma.
Kikao hicho kimekutanisha wadau mbalimbali ikiwemo katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, wakuu wa wilaya zote, Wakurugenzi wa Halmashauri zote, Makatibu Tawala wa Wilaya na Mameya wa Halmashauri zote, Viongozi wa dini, wadau kutoka TFF, TANROAD,TARURA, UDART, DAWASA, TANESCO pamoja na wadau wengine kutoka Sekta binafsi.





Post a Comment