Na Jackson Joseph Nyasebwa – DAR ES SALAAM
WATAALAM wanaoshiriki katika maandalizi ya Mpango wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori wamepatiwa mafunzo ya ufahamu wa malengo ya Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uelewa wao kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma na namna ya kuyatekeleza kwa kuzingatia mahitaji ya wakati uliopo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Novemba 3. 2026 katika ukumbi wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam yanalenga kuwajengea washiriki uelewa wa dhana ya malengo ya taasisi za umma na umuhimu wake katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi pamoja na uhusiano uliopo kati ya malengo ya taasisi hizo na matokeo yanayotarajiwa katika utekelezaji wa mipango, mikakati na programu mbalimbali za Serikali.
“Lengo ni kauli inayoeleza matokeo au manufaa ambayo mteja au mnufaika wa huduma anatarajiwa kuyapata kupitia utoaji wa huduma au bidhaa. Hivyo, Serikalli na taasisi zake zinapaswa kuhakikisha kuwa malengo yake yanajielekeza katika kutatua changamoto za wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma,” amesema
Dkt. David Manyanza, amesisita kuwa wakati huu ambao Wizara za kisekta na taasisi zake zinaanda Mpango wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori, ni muhimu kwa watalaamu wanaotengeneza mpango huo kuzingatia mahitaji ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za migongano hiyo, hususani katika kubuni mikakati itakayolinda maisha ya watu, mali zao na rasilimali za wanyamapori.
Aidha, washiriki walielekezwa kuhusu umuhimu wa kuelewa malengo ya taasisi wanazotoka na namna malengo hayo yanavyopaswa kuendana na malengo ya Serikali katika kushughulikia migongano baina ya binadamu na wanyamapori kwa kuwa uelewa huo utasaidia watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuweka vipaumbele sahihi na kuhakikisha kuwa shughuli zinazofanyika zinachangia kufikia matokeo yaliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alex Lobora, akichangia hoja alisema,“…Mafunzo ya leo yametuwezesha kuelewa umuhimu wa kuoanisha malengo ya taasisi na huduma zinazotolewa kwa wananchi, kwa kuzingatia kuwa mafanikio ya taasisi za Serikali hayapimwi kwa idadi ya shughuli zinazotekelezwa pekee, bali pia kwa matokeo na manufaa yanayopatikana kwa walengwa wa huduma hizo.”
Kupitia mafunzo hayo, watalaamu wanatarajiwa kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha maandalizi ya Mpango wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori ili uweze kuendana na malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi, kupunguza athari za migongano baina ya binadamu na wanyamapori na kuimarisha ustawi wa jamii pamoja na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori nchini.
Mpango wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa changamoto zinazojitokeza kati ya wananchi na wanyamapori katika kipindi cha utekelezaji wa miaka 10 kuanzia Mwaka wa Fedha 2026/2027 hadi 2036/2037 huku mkazo ukiwekwa katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza.






Post a Comment