Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe
Dkt Angeline Mabula akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka
taasisi ya Zawadi Initiativi.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe
Dkt Angeline Mabula akimkabidhi cheti moja ya wahitimu wa mafunzo ya
ujasiriamali kutoa taasisi isiyo ya serikali ya zawadi initiative
....................
Wananchi wametakiwa kumshukuru na kumpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan kwa juhudi zake za
kuhakikisha unakuwepo usawa wa kijinsia, haki na ukombozi wa kiuchumi kwa
jinsia zote
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela
ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe
Dkt Angeline Mabula wakati wa kuhitimisha mafunzo ya ujasiriamali kwa mabinti
waliokosa elimu katika mfumo rasmi yaliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali
ya Zawadi Yangu Initiative iliyoko kata ya Mecco wilaya ya Ilemela katika
ukumbi wa Mtena ‘B’ Buzuruga.
Amefafanua kuwa jamii haiwezi kuwa na kizazi chenye
usawa kama hakuna chombo kinachosimamia suala hilo kwani kumekuwepo na vyombo
na majukwaa mbalimbali ya kupigania usawa lakini yameshindwa kufikia malengo
hivyo kitendo cha Rais Mhe Samia Suluhu Hasan cha kukusudia kutengenisha wizara
ya afya na maendeleo ya jamii kuwa wizara mbili tofauti ni cha kuungwa mkono na
kupongezwa kwani kitaongeza kasi ya usimamizi wa masuala hayo.
‘.. Kutenganisha
wizara hii ni jambo linaloenda kuweka mabadiliko chanya, Tutaenda kuona kasi ya
maendeleo kwa kugusa jinsia zote katika utendaji, Tunapozungumzia masuala ya
uwezeshaji kiuchumi na kuleta usawa wa kijinsia maanake sasa tutakuwa
tumeyagusa makundi yote lakini anaelengwa zaidi ni mwanamke ambae kidogo
amekuwa nyuma katika mambo mengi..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula ameongeza kuwa Serikali ya Rais
Samia imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kumkomboa mwanamke ikiwemo
kuendelea kutoa elimu bila malipo, kutoa fursa kwa mabinti watakaopata ujauzito
kwa bahati mbaya kuendelea na shule kama sheria na sera itakavyoelekeza, pamoja
na kufuta tozo zaidi ya 108 zilizokuwa kero katika masuala ya umiliki wa ardhi
na nyanja nyenginezo
Kwa upande wake afisa maendeleo wa manispaa ya
Ilemela Ndugu Sitta Singibala amewataka wahitimu hao kutobweteka na elimu
waliyoipata badala yake wajiunge katika vikundi ili waweze kukopesheka na
kujikwamua kiuchumi huku Diwani wa kata ya Buzuruga Mhe Manusura Sadick
akiwahakikishia ushirikiano katika kuhakikisha wanakuwa na mazingira rafiki ya
kujiajiri na kujiletea maendeleo
Akihitimisha mratibu wa mpango huo kutoka kituo cha
Zawadi Yangu Initiative Bwana Atiupele Amon Mwakitalu amesema kuwa mafunzo hayo
yametolwa bure bila gharama zozote na jumla ya mabinti 44 wamehitimu mafunzo
hayo huku 12 wakishindwa kufuzu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata
ujauzito na umbali kutoka makazi wanayoishi.
Grace Jeremiah ni moja ya wahitimu wa mafunzo hayo ameishukuru taasisi ya Zawadi Initiative kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwani yatawasaidia katika kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira pamoja na kuleta ushindani katika soko.
Post a Comment