BOT KUBADILISHA NOTI ZA ZAMANI KUANZIA JANUARI 2025


 Benki Kuu ya Tanzania(BOT), imetangaza kuondoa noti za zamani katika mzunguko, ikiwa ni pamoja na shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000), na elfu kumi (10000) za matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003, pamoja na noti ya shilingi mia tano iliyotolewa mwaka 2010.

Zoezi la kubadilishana noti hizi litaanza rasmi tarehe Januari 06, 2025 na kuendelea hadi Aprili 05, 2025. Watanzania watatakiwa kubadilisha noti hizo kupitia ofisi zote za Benki Kuu na benki za biashara, ambapo watapewa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.

Matumizi ya noti hizi yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali kuanzia Aprili 06, 2025. Tarehe hiyo ikifika, mtu yeyote au taasisi itakayomiliki noti hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote. Aidha, benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizondolewa.

Aidha Benki Kuu inawataka wananchi kuzingatia tarehe hizi muhimu na kuhakikisha wanabadilisha noti zao kabla ya ukomo huo ili kuepuka usumbufu wowote.

0/Post a Comment/Comments