ZIJUE AINA ZA MIKATABA YA KAZI


 Picha kwa hisani ya mtandao 
***

Imeandikwa na wakili, Justine Kaleb

Ule msemo usemao kazi nzuri ukiwa hujaipata na huwa mbaya ukiwa nayo unaweza ukaonyesha uhalisia wakati unapaswa kufahamu ni aina ipi ya mkataba wa ajira uliosainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa.

Kwa mujibu wa sheria ya mikataba mkataba ni makubaliano kati ya pande mbili yenye nguvu ya kisheria kwa lugha nyingine makubaliano ambayo pande zote mbili zinawajibika kisheria. Mkataba ni moja ya mambo muhimu sana kati ya haki za mfanyakazi wakati mwingine kuliko hata kiasi cha fedha na marupurupu anayopaswa kulipwa. 

Mkataba wa kazi hutoa mwelekeo wa ajira ya mfanyakazi, huonyesha usalama wa ajira, haki na wajibu wa mfanyakazi pamoja na haki na wajibu wa mwajiri, kueleza majukumu ya msingi ya mfanyakazi, muda na mahali pa kazi na maswala mengine muhimu kwa mujibu wa sheria. 

Kukosekana kwa mkataba wa kazi huhatarisha usalama wa ajira yenyewe. Hivyo ni wajibu wa kila mwajiri na mwajiriwa kuhakikisha anapata mkataba wa ajira ikiwezekana hata kabla hajaanza kufanya kazi yenyewe na kulipwa mshahara wake wa kwanza.

Pamoja na uwepo wa kipindi cha matazamio (probation period) lakini hilo haliondoi wajibu wa kuwepo kwa mkataba wa kazi. Baadhi ya waajiri wasio waaminifu wamekuwa wakitumia kipindi cha matazamio kama kigezo cha kutompa mfanyakazi mkataba wa kazi bila kutambua kwamba inawezekana kabisa mtu akasaini mkataba wa kazi na mkataba ukaeleza kuwa kipindi cha matazamio kitakuwa ni cha muda gani japo kisheria hakipaswi kuzidi miezi sita. Pia ndani ya kipindi cha matazamio mwajiri anayo haki ya kusitisha mkataba wa kazi endapo hataridhishwa na utendaji wa mfanyakazi au kwa sababu nyingine zozote zinazokubalika na ambazo ni halali kisheria. 

Aina ya mkataba wa kazi huonyesha mustakabali wa kazi yenyewe, humpa mfanyakazi na mwajiri fursa ya kufahamu haki na wajibu wa kila upande na hivyo kujenga mazingira mazuri ya utekelezwaji wake kwa kulinda maslahi ya kila upande.

Mkataba wowote ule unaoingiwa kati ya pande mbili ni lazima uwe na vigezo vikuu vya mkataba ikiwemo makubaliano ya pande mbili, malipo halali, lengo halali, uwezo wa kuingia mkataba na hiari. Bila kujali ni aina ipi ya mkataba wa kazi mliosaini, kama kimojawapo kati vigezo vikuu vya uhalali wa mkataba kitakosekana kinaweza kuufanya mkataba wenyewe kuwa batili tangu mwanzo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 mikataba ya ajira iko ya aina tatu ambayo ni; Mkataba usiokuwa na muda maalum, mkataba wa muda maalum kwa wataalam na kada ya uongozi pamoja na mkataba wa kazi maalum. 

Mkataba usiokuwa na muda maalum ni mkataba ambao unasainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa ambao unaweza kuonyesha tarehe uliyosainiwa lakini hauonyeshi au hauelezi kuwa utaisha lini. Mikataba ya namna hii mara nyingi huwa katika taasisi za umma na baadhi ya taasisi binafsi.

Aina ya pili ya mkataba wa kazi ni mkataba wa muda maalum kwa kada ya uongozi.  Aina hii ya mkataba huusisha zaidi kada ya uongozi au mwajiriwa mwenye fani ya aina fulani ambaye huajiriwa kushika wadhifa fulani wa juu katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Hata hivyo aina nyingine za waajiriwa wanaweza pia kuwa na mkataba wa muda maalum bila kujali kada anayotoka kulingana na mahitaji maalum ya mwajiri.

Aina ya tatu ya mkataba wa kazi ni mkataba  kwa kazi maalum. Mkataba huu unaweza kupewa kipindi maalum cha kuisha au mara nyingi kuisha kwake hutegemea kuisha kwa kazi husika ambazo mwajiri na mwajiriwa watakuwa wamekubaliana kutekeleza. 

Hii yaweza kuhusu utekelezaji wa mradi Fulani au shughuli maalum ambayo kuisha kwake ndiyo huashiria kufikia mwisho kwa mkataba wa ajira.

Jambo la muhimu na la kuzingatia ni kwamba kifungu cha 15 cha sheria ya ajira na mahusiano kazini, 2004 kinamtaka kila mwajiri na mwajiriwa kuhakikisha kuwa kabla ya kuanza kazi, kuna mkataba wa maandishi uliosainiwa kati ya pande hizo mbili. 

Pamoja na uwezekano wa kuwepo na makubaliano kati ya mwajiri na mfanyakazi ya kuwa na mkataba ulio chini ya mwaka mmoja lakini makubaliano hayo yanapaswa yafanyike kwa sababu za msingi na si kwa lengo la kujaribu kumnyima mfanyakazi baadhi ya haki zake zilizopo kisheria. Baadhi ya waajiri huingia kwenye makubaliano mapya ya mkataba na mfanyakazi kila baada ya miezi mitatu au sita ili kukwepa baadhi ya gharama zikiwemo kodi na malipo watakayowajibika kumlipa mfanyakazi kwa mujibu wa sheria jambo ambalo halikubaliki kisheria.

Mkataba ndio utakaoeleza aina ya shuguli utakazofanya, mipaka, unawajibika kwa nani, malipo yako, haki zako za msingi, namna ya kuvunja mkataba na maswala mengine muhimu ambayo hamuwezi kukubaliana tu kwa maneno. Kukosekana kwa mkataba wa maandishi kunahatarisha ulinzi na usalama wa haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa. Usikubali kuanza kazi bila mkataba. 

Usikubali kusaini mkataba bila kuusoma na kuuelewa na pia ni muhimu kujua umeingia mkataba wa aina gani kati hizo aina tatu nilizoeleza hapo juu, ili ujue haki na wajibu wako kisheria na namna gani maslahi yako kama mwajiri au mwajiriwa yanaweza yakalindwa pasipo vikwazo vya aina yoyote. 

ADVOCATE JUSTINE KALEB
CEO/LEGAL CONSULTANT
MORIAH LAW  CHAMBERS,
MAVUNO HOUSE - POSTA MPYA,
(OPPOSITE TO TOTAL PETROL STATION),
1ST FLOOR - OFFICE NO. 102,
P.O. BOX 70849,
DAR ES SALAAM - TANZANIA - EAST AFRICA.
MOB: +255 755 545 545 600 / +255 713 636 264
TEL: +255 222 110 684
EMAIL: moriahclients@gmail.com
FACEBOOK: Moriah Law Chambers

0/Post a Comment/Comments