MGOMBEA WA CCM AIBUKA MSHINDI UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE JIMBO LA NGORONGORO


Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ngorongoro, Dkt.Jumaa Mhina (Kushoto) akikabidhi cheti cha ushindi wa Kiti cha Ubunge kwa Mbunge Mteule wa Jimbo la Ngorongoro, Bw. Emmanuel Lekishon Shangai baada ya kuibuka mshindi kwa kupata kura 62,017 Kati ya kura 62,528 zilizopigwa katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika Desemba 11,2021.

.......................

Mgombea Ubunge Jimbo la Ngorongoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw. Emmanuel Lekishon Shangai ametangazwa mshindi kwa kupata kura 62,017 Kati ya kura halali 62,461 katika Uchaguzi Mdogo wa jimbo hilo uliofanyika tarehe 11 Desemba, 2021. 

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo Dkt.Jumaa Mhina  amemtangaza Bw. Shangai kuwa mshindi siku Jumapili Oktoba 12, 2021 katika kituo cha majumuisho ya kura kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha. 

Katika matokeo hayo, Shangai amefuatiwa na mgombea wa Chama Cha ACT Wazalendo, Johnson Mahuma Gagu, aliyepata kura 170 kati ya kura 62,528 zilizopigwa. 

Mgombea mwingine katika uchaguzi huo Saimin Paul Ngilisho wa Chama cha Demokrasia Makini alipata kura 105 na Mohamed Kitundu wa Chama cha ADC alipata kura 63 huku mgombea wa Chama cha ADA TADEA Mwinyi Hamisi akipata kura 30. 

Aidha katika Uchaguzi huo ulikua na Wagombea  kutoka Vyama vya Siasa 11 ambapo vyama vingine vilivyopata kura katika Uchaguzi huo Mdogo uliofanyika Desemba 11, ni Mary Moses Daud wa UPDP aliyepata kura 20 huku Wagombea wa Juma Feruziyson wa NRA na Amina Amir Mcheka wa NLD walipata kura 16 kila mmoja. 

Mwita Makuru wa Chama cha UDP alipata kura kumi huku Saimon Johnson wa SAU aliyepata kura tisa (9) na Frida Marko Nko wa UMD akipata kura tano (5). 

Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Ngorongoro umefanyika baada ya aliyekua Mbunge wa Jimbo hilo, William Ole Nasha kufariki dunia.

0/Post a Comment/Comments