Wakulima 72 wa Mkoa wa Katavi wamenufaika na mafunzo
ya matumizi sahihi ya mbolea baada ya wataalam kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa
Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na wadau wake kutoka
kampuni la mbolea la OCP Tanzania Ltd na wazalishaji wa mbegu wa Seedco kutoa
mafunzo hayo kwa wakulima.
Mafunzo na uhamasishaji huo wa matumizi sahihi ya
Mbolea umefanyika tarehe 17 Januari, 2024 katika Halmashauri ya Manispaa ya
Mpanda katika kata ya Magamba na Kakese ambapo jumla ya wakulima 46
wamehamasishwa juu ya matumizi sahihi ya Mbolea.
Awali, wakulima 26 wa kata ya Katuma kijiji cha
Kapanga Halmashauri ya Wilaya Tanganyika walifikiwa na elimu hiyo na kufanya
jumla ya wakulima 72 waliofikiwa na
elimu ya matumizi sahihi ya Mbolea katika wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mafunzo hayo, Mkulima PIASON
KALWIHO MTAFYA wa Kijiji cha Kapanga kata ya Katuma Wilaya ya Tanganyika,
mkoani Katavi, ameishukuru Serikali kwa Kuja na mpango wa ruzuku na kueleza
mpango huo umeleta nafuu kubwa kwa wakulima kwa awali walikuwa wakununua mbolea
kwa bei kubwa ya shilingi 150,000 ambapo wakulima wengi hawakumudu na hivyo kuzalisha kidogo.
Ameishukuru TFRA na washirika wake kwa kuja na
mpango wa kuwaelimisha kupitia mashamba darasa na kueleza imesaidia kuondoa
mtazamo hasi waliokuwa nao kuwa, mbolea inaharibu udongo.
Sambamba na mafunzo hayo, Kanda hiyo inaendelea na mafunzo katika mikoa ya Njombe, Songea na wilaya za Ludewa Tunduru kata ya Nakayaya wakiwa na lengo la kuwafikia wakulima 500 Katika Mikoa 7 Halmashauri 40 za Nyanda za Juu kusini.
Post a Comment