Na Sixmund Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa wito kwa Vyombo vya Habari nchini kuhamasisha watanzania waliopo ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu kwenye kampeni maalum ya “vote now” inayoendelea ya kuvipigia kura vivutio vya utalii ili vishinde Tuzo za World Travel Awards mwaka huu
Vivutio hivyo ni Hifadhi za Taifa za Serengeti, Kilimanjaro na Ngorongoro ambavyo vimeweza kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo za World Travel Awards ambapo zaidi ya vivutio 100 vinashindanishwa kwa katika makundi tofauti.
Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele ametoa wito huo mkoani Iringa wakati alipokuwa akihojiwa na Waandishi wa Habari kwenye Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imepata mafanikio makubwa katika Sekta ya Maliasili na Utalii ambapo amefafanua kuwa kumekuwa na Kuongezeka kwa idadi ya watalii ambapo idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 Mwaka 2023.
Aidha, idadi ya Watalii wa Ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 152 kutoka watalii 788,933 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,985,707 Mwaka 2023, rekodi kubwa ambayo haijapata kufikiwa katika kipindi chote tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania.
Pia kumekuwa na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii ambapo mapato yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 161 kwa watalii wa kimataifa. Aidha, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 175.3 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 279.
Aidha, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali uliongezeka kutoka Shilingi 397,428,671,968 Mwaka 2020/2021 hadi Shilingi 680,150,218,337 Mwaka 2022/2023. Vilevile, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kuanzia Julai 2023, hadi kufikia Aprili 2024, Wizara imekusanya jumla ya Shilingi 750,992,839,479.75 sawa na asilimia 97.12 ya lengo la makusanyo. Makusanyo haya pia ni rekodi ya juu ya mapato kuwahi kuwekwa katika Sekta hizi Nchini.
Tully Kulanga, Afisa Utalii Mkuu (Kanda ya Nyanda za Juu Kusini) amesema ongezeko hilo la wageni limetokana na jitihada mbalimbali za serikali katika kuendeleza sekta ya utalii ikiwemo utekelezaji wa mradi wa REGROW.
“Tumekuwa tukiongeza mazao mapya ya utalii ambayo ni pamoja na utalii wa fukwe, utalii wa meli, utalii wa treni na utalii wa michezo,” amesema na Kulanga na kuongeza kuwa lengo la serikali ni kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025.
Afisa Utalii Mwandamizi kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Nyanda za Juu Kusini, Sane Tobico amesema wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kutangaza vivutio vya utalii. Amesema ujenzi wa kituo cha kutangaza utalii mikoa ya kusini kupitia mradi wa REGROW utasaidia zaidi kuongeza idadi ya watalii.
Tobico ameongeza kuwa bodi imekuwa ikiwatumia watu maarufu kuja kutembelea vivutio vilivyoko nyanda za juu kusini kwa ajili ya kuvitangaza kote duniani.
Post a Comment