Na Daniel Limbe, Chato
MKURUGENZI wa huduma za matibabu kwenye hospitali ya rufaa ya Kanda Chato,Dkt. Osward Lyapa,amesema suala la wataalamu wa saikolojia bado ni changamoto kubwa nchini licha ya umuhimu wao hasa kwenye kada ya afya pamoja na jamii kwa ujumla.
Ni kutokana na uwezo wao mkubwa wa kutoa ushauri tiba hasa pale mtu anapokuwa amezongwa na hali isiyokuwa ya kawaida ikiwemo majonzi kupita kiasi,mifarakano na kukata tamaa kwa kushindwa kuhimili mambo yanayomsibu kwa wakati.
Dkt. Lyapa ambaye pia ni Bingwa wa Magonjwa ya wanawake ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na mwandishi wetu ambapo amedai mbali na jamii kuwachukulia madaktari kama watu wenye uwezo na ujuzi wa kuhimili mambo magumu,bado kundi hilo linahitaji kuwa karibu zaidi na wasaikolojia tiba Ili waweze kutimiza majukumu yao vyema.
"Kwa muda mrefu jamii yetu imekuwa ikituchukulia madaktari kama watu tunaoweza kuhimili mambo magumu,mtazamo huo siyo kweli ni muhimu ifahamike kuwa daktari naye ni mtu kama wengine anaweza kufadhaika na kushindwa kuhimili mambo mazito yanayotokana na kazi yake".anasema Dkt. Lyapa.
"Kuna wale wenye magonjwa ya muda mrefu kama kansa unaweza kumhudumia mpaka mnakuwa marafiki wa karibu,lakini inatokea anafariki dunia hali hiyo huwa inatuumiza sana, na unapokosa msaikolojia karibu inaweza kusababisha kuingia kwenye unywaji wa pombe ukiamini inaweza kukupunguzia mawazo na uchungu".
Anasema licha ya kazi kubwa inayofanywa na serikali kuhakikisha inawasomesha wataalamu wa saikolojia tiba ikiwa ni mpango mkakati wa kuwa na vitengo maalumu nane kwenye kila hospitali ya rufaa ya mkoa na Kanda,bado jamii kubwa inaendelea kuhudumiwa na viongozi wa dini wakiwemo Mapadri,Wachungaji, Mashekhe,wazee maalufu na waganga wa jadi.
Mpango huo unakusudia kuongeza idadi ya wataalamu ambao watakuwa bingwa na wale wabobevu ili kuhakikisha huduma zilizokuwa zikipatikana kwenye hospitali kubwa zilizoko mbali na maeneo yao sasa ziwafikie kwa ukaribu zaidi, hatua itakayo wapunguzia wananchi gharama za kusafiri na kuuguza wagonjwa wakiwa mbali na makazi yao.
"Kwa muda mrefu jamii yetu imekuwa ikihudumiwa na viongozi wa dini,Mapadri,Mashekhe,viongozi maarufu wa Mila pamoja na waganga wa jadi,makundi hayo ndiyo yalishikilia taaluma hiyo kutokana na jamii kuamini kuwa watu hao huenda wamekutana na misukosuko mingi katika utatuzi wa masuala ya kijamii".
"Ni muhimu itambulike kuwa Saikolojia tiba ni taaluma inayosomewa darasani na kwamba jamii inatakiwa kueleweshwa namna ya kuwapata wataalamu hao ili wakiona mtu anachangamoto kama hizo wajue wanapaswa kumpeleka wapi ambayo itakuwa ni sehemu sahihi" anasema Dkt. Lyapa.
Mbali na wataalamu wa saikolojia,pia anapendekeza kuongezwa kwa idadi ya madaktari wa Afya ya akili kwa kuwa baadhi ya mambo yasiyofaa katika jamii yamekuwa yakifanywa na watu wenye changamoto hiyo huku jamii ikiona kama hali ya kawaida.
"Sisi madaktari tumekuwa mstari wa mbele sana kuwasemea wananchi kwa changamoto zao za afya ya akili na saikolojia,lakini sisi ninani anayetuongelea tunapo pata shida kama hizo" anahoji Dkt. Lyapa.
Mwisho.
Post a Comment