.......................
WANAFAMILIA wawili wa Familia ya Zuberi Mtemvu, Ibrahim Mtemvu na Jasmin Mtemvu wamemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi kuingilia kati na kutatua mgogoro wa madai ya nyumba mbili za urithi Masaki na Temeke wanazodai zimeuzwa na ndugu yao Abbas Mtemvu bila wao kupata haki yao.
Akizungumza Dar es Salaam siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaapisha baadhi ya Mawaziri aliowateua hivi karibuni akiwemo Waziri Ndejembi kuwa Waziri wa Ardhi, Ibrahim amesema mgogoro huo uliodumu kwa takribani miaka mitatu wanaamini Waziri huyo anao uwezo wa kuumaliza.
Amesema kimsingi kaka yao huyo mkubwa katika familia, amejinufahisha mwenyewe na mauzo ya nyumba hizo jambo lililozua mgogoro huo huku akidai wao kuwa na nyaraka na ushahidi wote wa nyumba hizo mbili zilizouzwa kwa watu tofauti.
"Malalamiko yetu haya kwa mtu huyu ni ya muda mrefu, tunaona kama limegubikwa na danadana nyingi hivyo tunaamini tukipata nafasi ya kumueleza Waziri anaweza kutusaidia kupata haki yeti" alisema Ibrahim
Amesema wanachoona wao nafasi ya kisiasa aliyenayo kaka yao huo pamoja na wadhifa mbalimbali alizozipitia ndiyo zinazochelewesha wao kupata haki yao wakisisitiza kitendo alichofanya ndugu yao huyo siyo cha kiungwana hivyo hakipaswi kuachwa.
"Sisi hatuna nguvu za kutuwezesha kufanya chochote kwa mtu huyu kwa mwenzetu ana nguvu kifedha, njia pekee ambayo tunaona ni Waziri na wataalam wake pamoja na wadau mbalimbali hasa taasisi za haki za Binadamu kutusaidia katika hili" alisisitiza Ibrahim.
Aidha Ibrahim alisisitiza kwa kumuomba Waziri huyo kuanza na mgogoro huo mara wakiamini aanzapo majukumu yake ndani ya Wizara hiyo kwa madai ya kutokana na migogoro mingi iliyopo katika sekta ya ardhi baadaye nafasi ya kiongozi kulishughilikia suala lao litakuwa na changamoto nyingi.
Amesema tangu kuondolea kwao kwa nguvu katika nyumba ya Masaki na kisha nyumba hiyo aliyokuwa akiishi, maisha yake na wanafamilia wengine yamekuwa magumu , suala alilomuomba Waziri Ndejembi kulichukulia kwa uzito mkubwa kwa ajili ya kumnusuru yeye na wanafamilia wengine.
Alipotafutwa mlalamikiwa Abbas Mtemvu kupitia simu yake ya Mkono hakuweza ushirikiano baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa na kupitia kwa wakili wake..........
Aidha akizungumza mara baada ya kuwaapisha katika Ikulu ndogo Dar es Salaam jana, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na maagizo kwa Mawaziri wengine alimtaka Waziri huyo mpya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kwenda kuendelea pale alipoishia Waziri aliyepita katika Wizara hiyo Jerry Silaa.
Alisema akiwa ndani ya Wizara hiyo kwa kiasi kikubwa Silaa aliweza kupambana na migogoro mingi iliyokuwepo ndani ya Wizara hiyo hivyo Ndejembi anapaswa kwenda kuongeza juhudi zaidi ya pale alipoishia mwenzake.
Kwa upande wake Waziri Ndejembi aliahidi kwenda kutekeleza yake yote ambayo Rais Samia amemuagiza huku akiwataka viongozi waliopo chini ya Wizara yake kumpa ushirikiano wa kutosha ili kwenda kutekeleza majukumu waliyonayo
Post a Comment