Na Mwandishi Wetu- Zambia
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili amefungua rasmi mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Utalii wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika (67 CAF) na kusisitiza nchi za Afrika kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya utalii na kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji katika Sekta ya Utalii.
Ameyasema hayo leo katika mkutano huo unaoendelea kwenye hoteli ya Radisson Blue jijiniLivingstone Zambia.
Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kuzungumzia mustakabali wa Sekta ya utalii Barani Afrika na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo hasa changamoto ya usafiri wa anga kuwezesha watalii kufika katika maeneo ya utalii na kuweka mikakati ya kukuza na kutangaza utalii wa Bara la Afrika.
Naye, Waziri wa Utalii wa Zambia, Mhe. Rodney Sikumba amesema mkutano huo ni fursa pekee kwa nchi za Afrika kuungana katika kushughulikia ipasavyo masuala yanayozuia ukuaji endelevu wa Sekta ya Utalii.
“Kwa muda, tumekuwa tukizungumza juu ya ustahimilivu na ukuaji endelevu wa Sekta ya Utalii kwa sababu ya kile kilichotokea mwaka 2019, wakati huu tunapaswa kuwa na suluhisho bora na sahihi kwa changamoto yoyote inayojitokeza kuzuia uendelevu wa Sekta ya Utalii” amesisitiza.
Pia, amesema inaridhisha kwamba takwimu za Baraza Kuu la 121 la Baromita ya Utalii Duniani zinaonyesha kuwa kwa robo ya kwanza ya mwaka 2024 Watalii wa Kimataifa walifikia asilimia 97% ikilinganishwa na waliofika kabla ya janga la UVIKO - 19 mwaka 2019.
Amesema pamoja na utalii kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya janga la UVIKO-19, nchi za Afrika hazitakiwi kurudi nyuma kuiendeleza na kuikuza sekta hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika ufunguzi wa mkutano huo unaondelea nchini Zambia.
Post a Comment