TFRA YAZINDUA KAMPENI YA"KILIMO NI MBOLEA" KUELEKEA MSIMU WA KILIMO 2024/25

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea TFRA Joel Laurent akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watumishi wa TFRA,Menejimenti na waongozaji wa Kampeni hiyo Mbinga Mkoani Ruvuma wakati akitambulisha rasmi kampeni ya ‘Kilimo ni Mbolea
Balozi wa Mbolea Msanii Abdallah Nzunda maarufu Mkojani .

.....................
 
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA imetambulisha rasmi kampeni ya ‘Kilimo ni Mbolea’yenye maono na malengo kwa wakulima katika kuelekea msimu wa kilimo wa mwaka 2024/25.

Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watumishi wa TFRA,Menejimenti na waongozaji wa Kampeni hiyo Mbinga Mkoani Ruvuma Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Laurent amesema Jina la kampeni hiyo limebeba maana halisi na ujumbe mahsusi unaotarajiwa kupelekwa kwa walengwa ambao ni wakulima wote nchini kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya Mbolea, matumizi ya visaidizi vya mbolea ikiwemo chokaa kilimo.

Aidha amesema lengo pia ni kuhamasisha usajili wa wakulima kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku sambamba na upimaji wa afya ya udongo.

"Tutahakikisha tunalenga mambo tofauti ikiwemo Kuhamasisha usajili wa wakulima kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku na kuuhisha taarifa, kwa wakulima waliosajiliwa"amesema Mkurugenzi Laurent 

Laurent amesema kuwa Kampeni hiyo inamuandaa mkulima kuanza msimu wa kilimo, kwa kupata taarifa muhimu zitakazomsaidia kuongeza mavuno, ikiwemo elimu ya matumizi sahihi ya Mbolea atakayoipata wakati wote wa kampeni hiyo na taarifa za upatikanaji na utoshelevu wa mbolea kwa bei himilivu ya ruzuku.

Amesema pia lengo ni Kuongeza matumizi ya mbolea kwa kuzingatia kanuni nne muhimu (4R’s) ambayo ni Chagua Mbolea sahihi, Tumia Mbolea wakati sahihi, Tumia kipimo sahihi cha Mbolea na kuWeka Mbolea sehemu sahihi ya mmea.

Pia amesema kuwa Kampeni hiyo inawakumbusha wakulima kujisajili kwenye mfumo ili waweze kunufaika na mbolea ya ruzuku huku ikiwahamasisha kujua umuhimu wa kutumia chokaa kilimo, kwenye udongo wenye tindikali/uchachu/nyongo ya kiwango cha juu(ph)ili kuirekebisha hali hiyo na kuyapa mazao nafasi ya kustawi vema. 

Mkurugenzi huyo amesema kuwa Kampeni hiyo inaanza wakati huu kuelekea kuanza msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, na hivyo inatarajiwa kufikia tamati mwezi Oktoba wakati wa kilele cha siku ya Mbolea Duniani itakayofanyika kanda ya Kaskazini katika Mkoa wa Manyara.    

Katika uzinduzi huo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea TFRA imemtambulisha msanii wa Komedi Abdallah Nzunda maarufu Mkojani kama Balozi wa Mbolea Ili kuhakikisha anaitangaza vyema na kuhamasisha matumizi ya Mbolea Kwa Wakulima.

0/Post a Comment/Comments