********
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amesema kuwa wapiga kura hao ni ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu uliopita na ambao watatimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Julai 20, 2024) alipozindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, katika uwanja wa Kawawa, mkoani Kigoma. Uzinduzi huo unaashiria kuanza kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchi nzima ambapo Mikoa inayoanza uboreshaji wa daftari hilo leo Julai 20, 2024 hadi Julai 26, 2024 ni Kigoma, Katavi na Tabora kisha mikoa mingine kufuata.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao. “Idadi hii si ndogo kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura hivyo nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa na mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa asisite katika vituo vya kujiandikisha tume imejipanga kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa popote walipo mpaka vitongojini”
“Nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine asisite kufika katika kituo cha kuandikisha kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa zoezi hilo lina lengo la kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata na kutumia haki yao ya kikatiba kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amelitaka Jeshi la Magereza kuweka miundombinu wezeshi ili kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutekeleza wajibu wake wa kuandikisha wafungwa wenye vifungo chini ya miezi sita na mahabusu kwa ufanisi.
“Hii fursa ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya kuwawezesha magereza kupiga kura ya kuchagua viongozi wanaowataka, hii mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kutoa fursa kwa wafungwa na mahabusu kupiga kura wakiwa magerezani”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia watanzania kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kuwa chaguzi zote zitakuwa huru na Haki.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiandanga amesema kuwa uzinduzi wa uandikishaji na uboreshaji, mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tume imekutana na wadau wa makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia,Viongozi wa Dini, Makundi Maalum kama vile Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu . Lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato huu unakuwa shirikishi kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa au dini”
Naye, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele amesema kuwa Jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar.
“Idadi hii ya vituo ni ongezeko la vituo 2,312 zaidi ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura kwa mwaka 2019/2020”.
(mwisho)
Post a Comment